Dereva mashakani kwa kuiba gari bandarini
Na BENSON MATHEKA
Dereva mmoja kutoka Mombasa alifikishwa katika mahakama ya Kibera akikabiliwa na shtaka la wizi wa gari la mfanyabiashara wa Nairobi, Nicholas Cheruiyot Rotich.
Bw Joel Mbithi Wanda ni mshukiwa wa tano katika kesi inayochunguzwa na maafisa kutoka makao makuu ya upelelezi jijini Nairobi.
Inasemekana alishirikiana na David Rono ambaye ni afisa wa forodha mjini Mombasa, Titus Buluma, Robert Kiprotich Bett na Judy Ndichu kupanga njama za kuiba gari la Bw Rotich la thamani ya Sh1.2 milioni.
Kulingana na shtaka ambalo alikanusha mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Barbara Ojoo gari hilo liliibwa Septemba 3, 2016, eneo lisilojulikana nchini Kenya. Sawa na washukiwa wengine Bw Wanda anakabiliwa na shtaka la pili la kuiba gari hilo aina ya Fielder.
Bw Rotich alidai aliagiza gari hilo kutoka ng’ambo na licha ya kuwasili nchini kupitia bandari ya Mombasa hakulipata. “Kwa pamoja na mkishirikiana na watu wengine ambao hawako kortini, mliiba gari la Bw Nicholas Cheruiyot Rotich lenye thamani ya Sh1.2 milioni,” lilisema shtaka.
Upande wa mashtaka uliomba kuunganisha kesi ya Bw Wanda na ya Bi Ndichu na ya washtakiwa wengine. Mahakama ilikubali ombi hilo na kuagiza Wanda kufika kortini Agosti 30 kesi yake iunganishwe na za washukiwa wengine. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000