• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:26 PM
Dini potovu: Familia lawamani kuua watoto saba

Dini potovu: Familia lawamani kuua watoto saba

NA PETER MBURU

Kuliibuka vioja wakati wa mazishi ya mtoto wa familia moja kutoka Nakuru Jumatano, baada ya wanakijiji kuwavamia na kuzua taharuki wakidai wazazi wa mtoto huyo walichangia kifo chake.

Wazazi wa Joram Nganga, mtoto wa miaka 14 walilaumiwa kwa kukosa kumpeleka mwanao hospitalini baada yake kuugua kifua kikuu wiki iliyopita, wakitaka aponywe na maombi.

Kulingana na majirani wa familia hiyo inayotoka eneo la Mzee wa Nyama, Pipeline huyo sasa ni mtoto was aba kuaga katika familia hiyo, na vifo vyote vimechangiwa na wazazi kukataa kuwapeleka hospitalini kupata matibabu.

Majirani walieleza Taifa Leo, wazazi hao ni waumini wa ‘Kanitha wa Ngai’ (kanisa la Mungu) ambapo Imani zao zinawakataza kutafuta matibabu hospitalini.

Familia hiyo inaripotiwa kukosa kumfikisha mwanao hospitalini kupata matibabu, licha ya hali yake ya afya kudhoofika, na badala yake ikaamua kumwombea ili aponywe na Mungu.

“Tunaliona kuwa jambo la kushangaza sana kuwa wanakataa kuwapa wanao matibabu lakini wanapokufa wanawapeleka mochari. Imani zao potovu sasa zinaadhiri maisha ya wanao kwani ni watoto wanaokufa,” akasema Bw Anthony Thiongo, jirani.

Familia hiyo imelaumiwa kwa kuwafungia watoto wao nyumbani badala ya kuwapeleka hospitalini kupata matibabu pale wanapougua.

Hata hivyo, babake marehemu alionekana kuridhika na kifo cha mwanawe kwani hakuwa na majuto, akikitaja kifo cha mwanawe kuwa ‘mpango wa Mungu’ na kurejelea kisa cha Ayubu katika Biblia ambaye aliwapoteza wanawe wote.

“Kifo cha mwanangu ni mpango wa Mungu na hivyo siwezi kukikosoa, hata Ayubu aliwapoteza wanawe wote na ulikuwa mpango wa Mungu,” akasema baba huyo.

Mambo yalipozidi unga, mzee huyo alichana mbuga, akishikilia kuwa anampenda mwanawe na kuwa aliridhika na kifo chake.

Nduguye baba huyo Bw James Karanja alilalamika kuwa hakufahamishwa kuhusu kifo wala mpango wa mazishi wa binamu yake, akieleza kuwa mbeleni amewahi kumpata mtoto huyo akiwa amefungiwa chumbani akiwa mgonjwa zaidi na akampelekea hospitalini.

Majirani aidha walikosoa hatua ya chifu kutoa kibali cha mazishi kwa familia hiyo, licha ya kfahamu kuwa kifo cha mtoto huyo kilitendeka katika hali ya kutatanisha.

“Majirani hawakuhusishwa kwenye mipango ya mazishi kwani ilifanywa kisiri na ndipo tunashangaa namna chifu alifikia uamuzi wa kuwapa kibali cha kumzika mtoto huyo,” Bw Thiongo akasema.

Wakazi sasa wanaitaka serikali kuingilia kati kuokoa maisha ya watoto wawili waliosalia katika familia hiyo, wakisema yamo hatarini.

Kulingana na mchuuzi katika kaburi la Nakuru North ambapo mtoto huyo alizikwa, ameiona familia hiyo ikifika kaburini humo kuwazika watoto mara nne tangu mwaka wa 2014 sasa, na sura zao ‘zimekuwa za kawaida’ eneo hilo.

Mazishi yaliendelea baadaye, baada ya wakazi na familia kuvurugana kisha umma ukaingilia na kuwasihi kutuliza hali.

  • Tags

You can share this post!

Utata kuhusu safari za Mecca Waislamu wakikosa paspoti

Kocha amsifu kinda kwa weledi wa soka

adminleo