Dongo Kundu: Serikali yatoa Sh100m kulipa walioathiriwa
Na WINNIE ATIENO
SERIKALI imetoa Sh100 milioni kufidia wamiliki wa mashamba walioathirika na ujenzi wa barabara kuu ya Dongo Kundu kaunti ya Kwale.
Halmashauri ya barabara kuu nchini, ilitangaza kuwa fedha za kuwafidia wote walioathirika na ujenzi huo zimetolewa kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) ambayo imeanzisha ukaguzi maalum kabla ya kuwalipa walioathirika na ujenzi huo.
“Kwa sasa tume ya Ardhi inafanya ukaguzi maalum kabla ya kufidia walioathirika na ujenzi huo. Hakuna hitilafu yoyote dhidi ya watakaofidiwa kwa hivyo tunawasihi muwe na subra,” alisema mkurugenzi wa mawasiliano katika halmashauri za barabara kuu nchini, Bw Charles Njogu.
Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, Bw Njogu alisema mwanakandarasi anamalizia maswala kadhaa ikiwemo kutathmini udongo na ardhi ambayo ni ya serikali katika shamba hilo.
“Mwanakandarasi anamalizia kazi yake katika awamu ya tatu. Tume ya ardhi imeshapokea fidia ya Sh400 milioni huku tukitayarisha bili ya awamu ya tatu Sh500 milioni,” aliongeza.
Alisema haya huku maafisa wakuu wa halmashauri hiyo wakitarajiwa kuzuru eneo la Pwani kudadisi ujenzi wa barabara kuu.
Hii ni afueni kwa wakazi wa Matuga na sehemu kadhaa kaunti ya Kwale ambao wamekuwa wakilalamika kwamba hawajafidiwa licha ya mashamba yao kuchukuliwa na serikali kwa aujenzi huo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bw Hamisi Tsuma Mwero, wakazi hao wamekuwa wakilalamika kwamba mashamba yao yanatumiwa kwa ujenzi wa barabara hiyo kuu ilhali hawajafidiwa.
Aidha wamekuwa wakiwalaumu machifu kwa kushindwa kushughulikia malalamishi yao.
“Tumeondolewa kwenye mashamba ambayo tulirithi kutoka kwa babu zetu, tumekuwa tukiendeleza ukulima kabla ya kufurushwa kwasababu ya ujenzi huu. Kile tunaomba ni fidia, sehemu hizo kuna makaburi ya babu zetu,” alisema Bw Mwero.
Seneta wa Kwale, Bw Issa Boy Juma pia aliitaka serikali ya kitaifa kuharakisha kufidia familia ambazo ardhi zao zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu huku akiishtumu NLC kwa kuchelewesha malipo hayo.
Aliitaka kamati ya seneti ya ardhi kuchunguza suala hilo kwa haraka ili waathiriwa wafidiwe.
Bw Juma alisema mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu tayari yuko kwenye eneo la kazi lakini familia bado hazijalipwa fidia.
“Ninasihi mamlaka husika kuhakikisha jambo linasuluhishwa na watu walioathirika wanalipwa kikamilifu kwa miradi iliyopo,” akasema.
Aliongeza kuwa mchakato wa fidia ni wa muda mrefu na familia husika kwa sasa zinakosa imani na uvumilivu.? Ujenzi huo utakapokamilika utatoa njia mbadala ya kufika Pwani ya Kusini ambapo kumekuwa na msongamano wa magari katika kivuko cha feri eneo la Likoni.