DPP akosolewa kumfungulia mashtaka wakili Nyakundi
Na RICHARD MUNGUTI
JARIBIO la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji la kumfungulia mashtaka ya mauaji wakili Assa Nyakundi liligonga mwamba Alhamisi..
Bw Nyakundi aliyetiwa nguvuni Jumatano na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Kamkunji Nairobi alifikishwa mbele ya Jaji James Wakiaga.
Mawakili wanaomtetea Dkt John Khaminwa, Harun Ndubi, Samson Nyaberi na Danstan Omari walipinga hatua ya naibu wa DPP Catherine Mwaniki kuwasilisha shtaka la mauaji.
Nyakundi ameshtakiwa kwa kosa la kumuua mwanawe bila kukusudia. Wakili huyo anadaiwa alimpiga mwanawe risasi na kumuua bila kukusudia.
Alipofikishwa mbele ya Jaji Wakiaga , Bi Mwaniki, aliwasilisha shtaka lakini Dkt Khaminwa akapinga akisema “kuna kesi nyingine mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Kiambu dhidi ya mshtakiwa ambayo haijakamilishwa.”
Dkt Khaminwa alisema hatua ya DPP kuwasilisha shtaka la mauaji dhidi ya wakili Nyakundi ilhali kuna kesi nyingine ambayo haijakamilika “ni ukandamizaji wa haki zake.”
Dkt Khaminwa alimweleza Jaji Wakiaga kuwa sheria ni kuwa kesi moja ikamilishwe kwanza kabla ya nyingine mpya kuwasilishwa.
Mawakili hao waliomba mahakama itoe uamuzi ikiwa mmoja anaweza kushtakiwa kwa kesi mpya ilhali nyingine sawa na hiyo ikiendelea.
Jaji Wakiaga aliamuru ombi iwapo DPP atawasilisha shtaka la mauaji itasikizwa leo. Nyakundi amekanusha shtaka la kumuua mwanawe Joseph , bila kukusudia Machi 2019.
DPP aliwasilisha ombi la kutamatisha kesi ya kuua bila ya kukusudia na kumfungulia shtaka jipya.
Uamuzi utatolewa mnamo Julai 5, 2019.