• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
DPP aonya polisi wanaoua vijana

DPP aonya polisi wanaoua vijana

Na MISHI GONGO

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, ameonya maafisa wa usalama wanaodaiwa kuteka nyara vijana wanaoshukiwa kuwa magaidi eneo la Pwani, ambao hupatikana baadaye wakiwa wameuawa na wengine hatima yao huwa haijulikani.

Alikemea pia mauaji ya kiholela ya washukiwa wa uhalifu eneo hilo akisema kuwa atakayepatikana akishiriki katika uovu huo atachukuliwa hatua.

Bw Haji aliwahimiza maafisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi nchini (ATPU) kufuata sheria katika kukabilianana washukiwa wa ugaidi.

Mkurugenzi huyo alisema si sawa kwa washukiwa kuteswa au kutolewa uhai kisha miili yao kutupwa misituni bila kuipa mahakama fursa ya kuwahukumu.

Mwezi Januari miili minne ya wanaume waliodaiwa kupotea baada ya kuchukuliwa na maafisa wa usalama katika Kaunti ya Kwale ilipatikana ikiwa na majeraha katika Mbuga ya wanyama ya Tsavo.

“Tunapaswa kutumia sheria kuangamiza ugaidi nchini. Tunawapongeza maafisa wote wale wanaosaidia katika viti hivi. Hatutasaza afisa yeyote atakayepatikana akishiriki katika unyanyasaji na au ukiukaji wa haki za kibinadamu,” akasema Bw Haji.

Akizungumza wikendi katika Shule ya Upili ya Sheikh Khalifa mjini Mombasa wakati wa sherehe ya kuwatuza vijana waliofanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa shule za upili KCSE mwaka uliopita, Bw Haji aliwashauri vijana kuwa wazalendo na kutoshawishika kujiunga na makundi ya kigaidi na ujambazi.

“Nyinyi ndio wajenzi wa taifa hili. Kama wazalendo hamupaswi kujihusisha katika shughuli zozote zitakazoiletea nchi hii maafa,” akasema.

Pia aliwaonya dhidi ya kushiriki katika ulanguzi wa dawa za kulevya akisema kuwa anaunga mkono mswada wa kukarabati kitengo katika katiba kinachozungumzia adhabu ya ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Alisema kupitishwa kwake ndio njia pekee ya kumaliza madawa hayo eneo la Pwani ambalo limetajwa kuwa kitovu cha biashara hiyo haramu.

Maneno yake yaliungwa mkono na Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, akisema kuwa mswada huo unalenga kuwapa wanaoshiriki katika biashara ya madawa ya kulevya adhabu kulingana na makosa yao.

Alieleza kuwa kipengee hicho kina mapengo na kinahitaji ukarabati ili kupambana na walanguzi vilivyo.

“Tunataka adhabu tofauti kwa walanguzi, wanaomiliki biashara hizo na wale watumizi, haiwezekani mmiliki na mtumizi kupewa adhabu sawa,” akasema mbunge huyo.

Bw Ali aliwashtumu mafisa wa kupambana na ugaidi kwa mauwaji ya kiholela yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo la Pwani.

Maeneo yaliyoathirika zaidi yakiwa ni Kwale, Mombasa na Lamu.

“Mshukiwa anafaa kukamatwa na kupelekwa mahakamani,akipatikana na hatia basi ahukumiwe kulingana na sheria na si kuadhiwa kishakutupwa misituni,”akasema.

Alieleza kuwa baadhi ya mafisa hao hutumia ugaidi, kulipizakisasi kwa kuwatoa uhai vijana wasiokuwa na hatia.

“Kuwaadhibu washukiwa hadi wakapoteza maisha yao kisha mkaitupa miili yao, hiyo si sawa. Afisa atakae onekana amekamata kijana kisha akatoweka, afisa huyo ndiye tutakae mshika atuonyesha alikompeleka mshukiwa naiwapo atapatikana amefariki basi atachukuliwa hatua,” akasema.

You can share this post!

Kanisa Katoliki laonya kuhusu kikundi potovu Nairobi

Ronaldo anavyompepesa Miss Bum Bum!

adminleo