EACC yalaumiwa kwa kujikokota kuchunguza sakata ya unyakuzi wa ardhi ya ADC Kilifi
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wameilaumu Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa kile wamedai ni kuwalinda watu mashuhuri waliohudumu katika utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi na ambao walitengewa sehemu ya ardhi ya Shirika la Ustawi wa Kilimo (ADC) katika Kaunti ya Kilifi.
Kamati ya Bunge Kuhusu Ardhi Ijumaa iliilaumu EACC kwa kutokamilisha uchunguzi kuhusu sakata hiyo licha ya uchunguzi huo kuanzia miaka 10 iliyopita.
Naibu mwenyekiti wa tume hiyo Sophia Lepucherit alikuwa na wakati mgumu kujibu maswali kutoka kwa wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kitui Kusini Dkt Rachel Nyamai waliomwekelezea maswali mazito huku akionekana kutokuwa na ufahamu wa kina kuhusu sakata hiyo.
“Sikuwa na habari kuhusu uchunguzi. Ni jana (Alhamisi wiki jana) ambapo nilielezwa kuhusu uchunguzi huo. Hata hivyo, nawahakikishia kuwa nitalifuatilia nitakaporejea afisini ili nifahamu sababu iliyofanya uchunguzi huo kujivuta kwa miaka mingi kiasi hicho,” akasema huku akikana madai kuwa EACC inajaribu kuficha ukweli kuhusu sakata hiyo.
Wanachama wa kamati hiyo walidai kuwa kuna maafisa fulani wa EACC ambao “huenda wanashirikiana na watu fulani” kuficha faili kuhusu uchunguzi huo kwa kutoa visingizio ambavyo havina msingi.
Ripoti
Kamati hiyo imetisha kuiwekea lawama tume hiyo itakapoandaa ripoti yake kuhusu sakata hiyo na kuiwasillisha bungeni wakati wowote wiki hii.
“Kama kamati tunashangaa kwamba kwa miaka 10 uchunguzi huu haujakamilishwa. Uchunguzi umecheleweshwa katika hali ambayo inaibua maswali mengi. Ni lini mtakamilisha uchunguzi huu?” akauliza Dkt Nyamai.
Mbunge wa Naivasha aliisuta EACC akidai ndiyo inaendeleza kero ya unyakuzi wa ardhi nchini.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mbunge wa Likoni Mishi Mboko alisema: “Licha ya EACC kufadhiliwa na pesa za mlipa ushuru bado imezembea katika masuala yanayohusu sakata za unyakuzi wa ardhi.”