EACC yalia kulemewa kufuatilia mali ya ufisadi, yasema ni ghali kupeleleza fedha zilizofichwa nje ya nchi
TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imefichua kuwa watu fisadi wameficha mapato ya ufisadi katika mataifa ya kigeni, na hivyo kufanya kuwa ghali kwa tume hiyo kuchunguza na kurejesha fedha hizo.
Mwenyekiti wa EACC, Askofu David Oginde alisema Jumapili kwamba tume hiyo haiwezi kuangazia kila sekta katika vita dhidi ya ufisadi kutokana na changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa fedha, ukosefu wa wafanyakazi wa kutosha, changamoto za kiufundi miongoni mwa nyingine.
“Kuchunguza ufisadi, hasa wa kiwango kikubwa, ni ghali sana. Kesi nyingi kubwa za ufisadi zinavuka mipaka ya kitaifa, kwa hivyo unapata pesa zilizoibwa nchini zinawekwa katika nchi nyingine na uchunguzi kama huo unahitaji maafisa kusafiri kwenda mataifa hayo na hiyo ni ghali sana,” akasema Askofu Oginde.
Alizungumza mnamo Jumapili katika kongamano la kila mwaka la biashara la Kanisa la CITAM jijini Eldoret. Askofu Oginde alisikitika kuwa licha ya juhudi za dhati za kupambana na ufisadi nchini kwa kila njia, ufisadi unaendelea kuenea nchini.
Alitaja ukosefu wa ufadhili unaotosha kuwa changamoto kuu inayozuia tume hiyo kupata mafanikio bora katika vita dhidi ya ufisadi.
“Bajeti tunayopewa haituwezeshi kufanya kazi yetu kwa uwezo wetu wote,” alisema Askofu Oginde na kuongeza kuwa tume ya EACC inachunguza visa kadhaa vya watu waliopata kazi hasa serikalini kwa kutumia vyeti ghushi.
Alisema watu kadhaa wenye vyeti feki wamefikishwa mahakamani huku tume ikitaka kurejesha fedha walizolipwa katika kipindi chote walichofanya kazi kwa kutumia nyaraka feki.
Alisema baada ya kulipa mamilioni ya fedha, washtakiwa hauchishwa kazi na kufunguliwa mashtaka husika.