• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Echesa kukaa bila bastola

Echesa kukaa bila bastola

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Waziri wa Michezo na Utamaduni Rashid Echesa anayeshtakiwa kwa kashfa ya ununuzi wa silaha ya Sh39 milioni ataendelea kukaa bila bastola zake mbili.

Echesa aliyeshtakiwa Machi 2020 kwa ulaghai wa mamilioni ya pesa aliwasilisha ombi arudishiwe gari lake la kifahari lenye thamani ya Sh23milioni, bastola mbili pamoja na kufunguliwa kwa akaunti zake.

Kupitia kwa mawakili Cliff Ombeta na Evans Ondieki, Echesa anadai anaumia na maisha yake yanakabiliwa na hatari kwa vile hawezi kusafiri baada ya kutwaliwa kwa gari lake.

Pia anadai akaunti zake za benki zilifungwa na “sasa anategemea marafiki kumsaidia kujimudu kimaisha.”

Hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot aliombwa na Echesa aamuru Serikali imfungulie akaunti zake, kumrejeshea bastola zake na kumrudishia gari lake.

Lakini mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Jacinta Nyamosi alipinga ombi hilo akisema “bastola hizo, gari na akaunti za Echesa ni ushahidi katika kesi inayomkabili.”

Uamuzi kuhusu ombi hilo ulipaswa kusomwa Ijumaa lakini hakimu hakuutayarisha kwa sababu ya kazi nyingi aliyokuwa nayo.

“Sikutayarisha uamuzi wa ombi la Echesa. Nilikuwa nashiriki katika mkutano kwa njia ya mitandao tangu asubuhi. Mikutano haifanywi kama zamani kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19. Tunashiriki mikutano kwa mtandao wa Zoom,” alisema Cheruiyot.

Hata hivyo alisema atausoma Juni 2, 2020.

Echesa amekana kuhusika na kashfa hiyo ya ununuzi wa silaha kutoka kwa kampuni moja ya Amerika.

  • Tags

You can share this post!

TANZIA: Mwanamuziki John Nzenze aliyevumisha...

Kwale yaibuka bora zaidi katika mpango wa ajira kwa vijana

adminleo