Habari Mseto

Ekeza Sacco yaanza kurejeshea wateja pesa zao

May 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na  MWANGI MUIRURI

EKEZA Sacco inayomilikiwa na Kasisi David Kariuki Ngari wa kanisa la Calvary Chosen Centre, Thika ambayo hivi majuzi iligonga vichwa vya habari kwa kuporomoka ikiwa na akiba za wateja kwa kima cha Sh2.4 bilioni imerejea tena kwa vichwa vya vyombo vya habari.

Mara hii sio kwa msingi wa jinsi kuporomoka huko kulimfaa Kasisi Ngari au mwingine yeyote katika kurebesha maisha na akiba hizo , bali
ni kwa taarifa njema kwa hao waliopoteza, watafidiwa.

Kasisi Ngari alitoa taarifa Alhamisi kuwa tayari alikuwa amezindua mpango wa kuwarejeshea wawekezaji waliokuwa wamehifadhi akiba ya Sh5,
000 kwenda chini.

“Hata nimewatumia barua za kuwafahamisha na pia walio na simu za mkononi tumewafahamisha kupitia jumbe fupi. Tunarejesha pesa zao
katika kanisa letu lililoko katika mtaa wa gatitu viungani vya mji wa Thika,” akasema Ngari.

Alisema kuwa ratiba ya kulipa pesa hizo huenda ikachukua miaka miwili.

“Nafanya hivi katika mazingira magumu sana. Serikali ilituharibia biashara na kwa sasa hakuna uzalishaji wa pesa ambao tunaendeleza kama
wafanyabiashara. Akaunti zangu nyingi zimefungwa na serikali imeweka vikwazo katika uamuzi wangu wa kuuza baadhi ya mali zangu ili kupata
pesa za kurejeshea wanachama wetu,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa kwa kuwa ana nia njema ya kurejeshea wanachama hao pesa zao, ataendelea mbele na kuwa mbunifu na akipata pesa kutoka kwa wale waliokuwa wamekopa kutoka kwa shirika hilo, awe akiwafidia wale ambao walikuwa wateja.

Upanuzi

Kwa mujibu wa aliyekuwa Kamishna wa Vyama vya Ushirika nchini, Bi Mary Mungai, shida kuu ya Ekeza ilikuwa katika upanuzi wake ambapo
licha ya kuwa na leseni ya kuhudumu katika eneo la Starehe Jijini Nairobi, kampuni hiyo ilipanua harakati zake hadi katika zaidi ya
Kaunti 10 hapa nchini.

Pia, Ekeza ikawa na kampuni ya kando na ambayo ni ile ya ununuzi na uuuzaji mashamba ya Gakuyo Real Estate na ambapo hakuna rekodi za
utendakazi zilikuwa zikiandaliwa kwa serikali kwa mujibu wa mwongozo wa vyama vya ushirika, hali ambayo ilizua changamoto kuu ya kupokonywa
leseni kwa muda.

Kupokonywa leseni kulizindua misururu ya washirika wa uwekezaji kuanza kutoa pesa zao kwa akaunti na ambapo shida za kifedha
ziliandama Ekeza kwa kasi kiasi cha kuzama.

“Hali inaweza ikalainishwa. Katika Ekeza, tulikuwa na hifadhi ya Sh2.5 bilioni za wateja lakini katika misukosuko iliyojiri, wanachama wengine wakatoa Sh500 milioni kutoka akaunti zao na hivyo basi tukajipata bila uthabiti wa uwekezaji,” akasema Kasisi Ngari.

Huku wanachama wengine wakizidi kusukuma warejeshewe pesa zao, Ekeza imelipa Sh116 milioni lakini katika Kampuni ya Gakuyo Real Estate
kukiwa na mikataba ya mikopo ya Sh1.3 bilioni.

“Hali hii inakuonyesha waziwazi kuwa tuko na changamoto ndio, lakini pia tuko na uthabiti wa kimsingi… Changamoto kuu ni kuwa majina ya
Kampuni zetu yameharibiwa sifa mitandaoni kiasi kwamba hata kupata mwekezaji wa kushirikiana naye kumekuwa na ugumu,” akasema Kasisi
Ngari.

Hata hivyo, alisema kuwa ako na matumaini kuwa mambo yatalainika baada ya kuonyesha wateja wake kuwa hakuna nia yoyote ya kuzamisha
akiba zao.