Elimu: Watoto wa wazazi walioyumbishwa kimapato na Covid-19 waomba ufadhili
NA SAMMY KIMATU
WATOTO wawili werevu kutoka familia maskini huenda wakakosa nafasi ya kujiunga na shule ya upili wiki ijayo kufuatia ukosefu wa karo.
Wanafunzi Edna Wanza Manzi,14, na Precious Ndulu,13, walizoa alama 410 na 414 katika mtihani wa KCPE 2023 mtawalia.
Wanza alikuwa akisomea katika shule ya Real Junior Academy, Mlolongo naye binti Precious katika Kyandu Academy, Kangundo.
Shule zote mbili ziko katika kaunti ya Machakos.
Mnamo Alhamisi, wazee wa Nyumba Kumi waliwapata watoto hao na wazazi na walipowaeleza kwamba ndoto ya watoto hao ya kusoma huenda ikakwama waliwachukua na kuwapeleka kwa mkuu wa tarafa ya Njiru katika kaunti ndogo ya Njiru, Bi Florence Syokau Mbwika.
Akiongea katika ofisi yake, Bi Syokau alisema watoto hao walizoa alama bora na wana maono ya kuendelea kusoma ili watimize ndoto zao.
Edna alilia akisimulia alivyojituma masomoni akilenga kupita mtihani wake licha ya kuwa mgonjwa mara kwa mara.
Msimamizi huyo wa tarafa ya Njiru alisema Edna amepokea barua ya kujiunga na Shule ya Upli ya Muthale Girls katika kaunti ya Kitui lakini changamoto kwake ni kwamba hakupata kartasi rasmi ya matokeo ya mtihani (Result slip) kwa sababu wazazi wake wanadaiwa Sh32,000 za malimbikizi ya karo.
“Mtoto Edna alifanikiwa kupata matokeo kwa njia ya kielektroniki kupitia simu ya babake. Hakuweza kupata kijikaratasi chenye matokeo hayo shuleni kwani wazazi wamelemewa kulipa Sh32,000 shuleni,” Bi Syokau akasema.
Kwa upande wa pili, Precious naye alizoa alama 414 na kupata barua ya kujiunga na shule ya upili ya Pangani Girls, Kaunti ya Nairobi.
Hayo hayawezekani kwa sababu shule inamdai Sh36,000 ili wazazi wake wapewe matokeo rasmi.
Watoto wote wawili walikuwa na ndoto ya kujiunga na uwakili, udaktari au uhandisi wakifanikiwa kumaliza kusoma chuo kikuu.
Wazazi wa Edna, Bi Jacinta Manthi, 36 na mumewe Geoffrey Manthi, 42 ni watu wa kuhamahama kwani walisaidiwa awali na kasisi wa kanisa la Rivers of God Peter Kisoi kupata hifadhi ya muda.
Kwao ni Mangelete, Nthongoni kaunti ya Makueni.
Kadhalika, wazazi wa Precious, Bi Miriam Peter Muendi na mumewe Boniface Mumo hawana kazi.
“Familia zote mbili zilipitia magumu baada ya wazazi wa pande zote mbili kufutwa kazini kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19 mwaka 2020,” Bi Syokau akasema.