• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
‘Embrace’, ‘Inua Mama’ wapata usemi mmoja

‘Embrace’, ‘Inua Mama’ wapata usemi mmoja

Na SAMWEL OWINO

VIONGOZI wanawake kutoka mirengo ya “Embrace” na “Inua Mama” wameapa kuweka kando tofauti zao na kuunga mkono mswada wa jinsia ambao umekosa kupitishwa bungeni mara tano.

Makundi hayo yalichipuka kuhusiana na siasa za 2022 ambapo ‘Embrace’ huunga mkono handisheki nao wale wa kundi la ‘Inua Mama” wako upande wa Naibu Rais William Ruto.

Wakiongozwa na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nyeri, Priscila Nyokabi, viongozi hao walisema hawatakata tamaa kuhakikisha mswada huo unapitishwa na kutekelezwa kikamilifu jinsi ilivyonakiliwa kwenye katiba.

Bi Nyokabi alisema watapinga mbinu zinazotumiwa na viongozi wa kiume kuwagawanya hasa nyakati ambapo mswada huo huletwa bungeni kupigiwa kura.

Mwenyekiti wa wabunge wa kike nchini (KEWOPA), Wangui Ngirici alisema wataendelea kuhakikisha hatua zilizopigwa katika upatikanaji wa haki za wanawake zitaendelea kuheshimiwa.

“Nia kuu ya mirengo yote miwili ni kuhakikisha mahitaji ya wanawake yanatimizwa. Pia tunaangazia uwakilishi sawa na kuwapa wanawake uwezo mkubwa wa kiuchumi,” akasema Bi Ngirici.

Wabunge wa mirengo hiyo miwili waliandaa kikao na wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi na kusema wamejitolea kuhakisha mswada huo unafaulu ukirejeshwa bungeni.

Waliohudhuria kikao hicho ni Gladys Wanga (Homa Bay), Florence Mutua (Busia), Rehab Mukami (Nyeri), Faith Gitau (Nyandarua), Esther Pasaris (Nairobi), Mary Seneta (Kuteuliwa), Rosa Buyu (Kisumu), Margaret Kamar (Uasin Gishu) na Fatuma Gedi (Wajir).

You can share this post!

Watetezi kimya Jubilee ikitatiza demokrasia, haki

Inspekta apatikana amefariki katika baa eneo la Bombolulu

adminleo