Eneo la Manguo, Ruiru kufunguliwa shule ya msingi ya umma
Na SAMMY WAWERU
KABLA mwezi huu wa Februari kufika tamati, inatarajiwa kwamba shule mpya ya msingi ya umma itakuwa imefunguliwa Manguo, katika eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.
Mbunge wa Ruiru Simon King’ara amesema shule hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya msingi ya umma ya Kimbo, iliyoko eneo la Progressive, wadi ya Kiu.
Akizungumza Alhamisi wakati wa uzinduzi wa madarasa mawili katika shule hiyo, Bw King’ara alisema Kimbo Primary ni mojawapo ya shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi nchini.
“Idadi ya wanafunzi katika shule hii ni karibu 2, 000 na ili kuipunguza tutazindua shule nyingine ya umma eneo la Manguo,” akasema mbunge huyo.
Ujenzi wa madarasa hayo ulifadhiliwa kupitia mgao wa fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF).
Kufunguliwa kwa shule ya Manguo pia kunatarajiwa kupunguza idadi ya wanafunzi katika shule ya Mwiki, Githurai. Aidha, shule inatajwa kuwa na zaidi ya wanafunzi 3, 000.
Mwaka 2019 Naibu wa Rais Dkt William Ruto alizuru Mwiki Primary na kuahidi kuzinduliwa ujenzi wa shule nyingine eneo la Manguo, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Hilo linajiri wakati ambapo kiwango kikubwa cha idadi ya wanafunzi katika shule za msingi za umma nchini kinaendelea kuwa gumzo, hasa kutokana na vifo vya wanafunzi 14 wa Kakamega Primary mapema wiki hii. Shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 3,000 ikiwa ni idadi kubwa.
Hata ingawa uchunguzi wa maafa hayo unaendelea, inasemakana walifariki katika kile kinatajwa kama kugutushwa na ‘kitu’, wakitoka madarasani ikizingatiwa idadi yao kubwa.