Habari Mseto

ERC inavyowaumiza watumizi wa mafuta taa

May 21st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Huenda mamilioni ya wananchi wakaathiriwa na pendekezo la Tume ya Kusimamia Kawi (ERC) kumaliza matumizi ya mafuta taa.

ERC ilitangaza azma ya kupandisha bei ya mafuta taa zaidi kwa lengo la kuwazuia raia wengi kutumia bidhaa hiyo.

Hata hivyo, bado mamilioni ya Wakenya hutumia taa za mafuta taa, maarufu kama ‘koroboi’.

Hii ni licha ya serikali kujikakamua kuhakikisha kila boma ina umeme. Mwezi  Aprili, Mkurugenzi Mkuu wa ERC Pavel Oimeke alisema serikali ilikuwa na mpango wa kuongeza bei ya mafuta taa ili ifanane na ile ya dizeli kwa lengo la kuwazuia watu kutumia mafuta taa.

Alisema kwa kuongeza ushuru kwa mafuta taa, serikali itakuwa na uwezo wa kuokota Sh354 bilioni na kulinda biashara za kuuza nje na magari kwa kuimarisha matumizi ya mafuta bora.

ERC inalenga kukuza matumizi ya sola na gesi katika kampeni ya kuimarisha mazingira.