EU kufadhili ujenzi wa viwanda 4 vya maziwa Tana River
NA STEPHEN ODUOR
MUUNGANO wa Ulaya (EU) umetia saini mkataba wa takriban Sh50 milioni na Kaunti ya Tana River unaonuia kujenga viwanda vinne vyenye mitambo ya kuhifadhi maziwa.
Juhudi hizo zinaenedelezwa chini ya mpango wa Maendeleo katika Maeneo Kame(IDEA).
Mitambo itawekwa katika kipindi cha miaka miwili katika maeneo ya Tana Kaskazini na Tana Delta, na inanuiwa kuinua uchumi katika kaunti na hata mapato kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.
“Mradi huu unakusudia kupunguza uharibifu ambao tumekuwa tukishuhudia kwa muda sasa kwa maziwa kuharibika,na pia kuimarisha uzalishaji tofauti na hapo awali ambapo wafugaji wamekuwa wakikadiria hasara kubwa,” alisema mkurugenzi wa idara ya mifugo, Bw Nzioka Wambua.
Bw Wambua alisema kuwa miradi hiyo itawekwa katika maeneo ya Bangale,Boka,Garsen na Odha,huku wanaolengwa wakiwa wafugaji wanaoishi au kulisha mifugo katika sehemu hizo.
Katika maeneo ya Bangale na Boka, mitambo hiyo itatumika katika ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa wafugaji,kuhifadhi kwa majokofu,na kuyatayarisha na kuweka kwa pakiti kabla ya kusafirisha maziwa hayo kwa soko za Garissa na Nairobi.
“Maziwa huwa rahisi sana kuharibika kwani ina sifa za kuvutia chochote katika mazingira,iwe harufu ya manukato,moshi na chochote kile na kisha kubadilisha ladha yake ikawa sawa na moshi au manukato husika,” alieleza Bw Wambua.
Aliongeza, “Hii ndio maana ni vyema tukipokea maziwa katika sehemu husika tuyachunguze kwana ili u tuhakikishe yako sawa kutumika na binadamu.”
Maziwa ya ngamia pia yatajumuishwa katika mpango.
itakayokuwa maeneo ya Bangale na Boka,huku eneo hilo likiripotiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita elfu kumi na mbili za maziwa kila siku.
Miji ya Garsen na Odha kwa upande mwingine inatarajiwa kuwa na mitambo hiyo katikati ya mji,huku kila mtambo ukitarajiwa kuweza kupokea lita elfu kumi kila siku,mbali na kuwa maeneo hayo yana uwezo wa kutoa zaidi ya lita elfu thelathini kwa siku.
“Watu katika sehemu hii hupata maziwa tele kila siku lakini maziwa hayo huharibika kwa wingi kwa kukosa soko ya moja kwa moja na mengine hutumika kwa matumizi ya nyumbani basi mradi huu utakuwa wa manufaa kwao sana kwani kipato chao kitakuwa na uhakika,”alisema Bw Wambua.
Pia alisema kuwa maziwa ya ngamia itanunuliwa kwa kati ya shilingi arobaini na shilingi sabini kwa kila lita,huku maziwa ya Ng’ombe yakinunuliwa kwa kati ya shilingi themanini na shilingi mia moja ishirini kwa kila lita ikilingana na msimu,kusudi likiwa ni kuwapa wafugaji kipato kutokana na bidii yao.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa miradi hiyo mbali na kuleta soko kwa zao la mziwa,pia itafungua njia za biashara na nafasi za kazi kwa wakaazi,kuwapa ujuzi katika uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na maziwa.
Vile vile ,mradi huo utafanikisha usafirishaji wa maziwa kutoka maeneo fiche palipo na wafugaji,na hata usafirishaji wa bidhaa hiyo kwa masoko tofauti tofauti nchini.
Wafugaji katika kaunti wamekuwa wakipata hasara kubwa kutoka kwa uuzaji na uzalishaji maziwa,huku bidhaa zao zikiharibikia njiani na wakati mwengine sokoni kwa kukosa wanunuzi.
Wanunuzi kwa upande mwengine wamekuwa wakisusia kununua maziwa hayo,ambayo huhifadhiwa katika vichupa vidogo ,kwa kuhofia usafi wa vyombo hivyo na jinsi zao hilo huhifadhiwa.