Habari Mseto

EU yamuunga mkono Rais wafisadi waadhibiwe vikali

January 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

MUUNGANO wa Ulaya (EU) umeunga mkono wito wa Rais Uhuru Kenyatta kutaka washukiwa wa ufisadi walioshtakiwa, wahukumiwe haraka.

Balozi wa EU nchini, Bw Simon Mordue Alhamisi alisema kuwa japo Idara ya Mahakama ina uhuru wa kufanya shughuli zake bila shinikizo kutoka nje, ni muhimu kwa taifa kuona wafisadi wakiadhibiwa.

Akizungumza mjini Nairobi baada ya kukutana na maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), balozi huyo alisema adhabu kwa washukiwa ndiyo itaashiria mafanikio katika kupambana na uporaji wa mali ya umma.

“Tunatambua uhuru wa asasi mbalimbali hasa mahakama, lakini tungependa mwaka 2020 uwe mwaka ambapo hukumu zinatolewa dhidi ya wafisadi, na mali za umma walizonyakua zinatwaliwa,” akasema.

Wakati Rais alitoa hotuba yake kwa taifa siku ya Jumanne akiwa mjini Mombasa, alisema juhudi za serikali yake kuangamiza ufisadi zimefanikiwa kuzuia wizi wa mali ya umma, kwani maafisa serikalini wanaogopa kukamatwa.

Lakini kwa mara nyingine, Rais alitaka Idara ya Mahakama iwajibike kwa kuhukumu haraka washukiwa wanaofikishwa kortini.

Shinikizo za kutaka mahakama iwahukumu washukiwa wa ufisadi zimesababisha mgogoro kati ya idara hiyo na serikali kuu.

Jaji Mkuu David Maraga husema hakuna jinsi kesi zinaweza kuharakishwa, kama upande wa mashtaka haujawasilishi ushahidi wa kutosha kwa wakati unaofaa.

Jana, Bw Mordue alisema adhabu kwa wanaopatikana na hatia ya ufisadi itasaidia pakubwa kupunguza uharibifu wa fedha za umma, ambazo badala yake zinaweza kutumiwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuboresha hali yao ya maisha.

“Twatumai kuwa tutaona watu wakihukumiwa kwa ufisadi ili wasirudi tena kushikilia nyadhifa katika ofisi za umma, wasiwe na uhuru wa kusafiri watakavyo. Ni kwa njia hiyo ufisadi utakomeshwa Kenya,” akasema, na kutaja ugaidi kama mojawapo ya matatizo yanayokumba Kenya kwa sababu ya ufisadi.

Balozi aliahidi kwamba mataifa ya EU yataendelea kuisaidia Kenya kupiga vita jinamizi la ufisadi, kwa hali na mali ikiwemo kutoa mafunzo maalumu kwa maafisa husika.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Twalib Mbarak alisema tume hiyo itaendelea kushirikiana na EU, huku mojawapo ya mahitaji muhimu zaidi katika ushirikiano huo ikiwa kusaka na kurudisha mali za umma zilizofichwa nchi za Ulaya.