• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Faini ya Sh500,000 kwa kumeza hongo ya Sh2,500

Faini ya Sh500,000 kwa kumeza hongo ya Sh2,500

Na RICHARD MUNGUTI

KARANI aliyeshtakiwa kupokea hongo ya Sh 2,500 katika Kituo cha kutoa Huduma  kwa wananchi cha Kibera kaunti ya Nairobi Alhamisi alitozwa faini ya Sh500,000 ama atumikie kifungo cha miaka miwili jela.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi (ACC) Bw Douglas Ogoti , alimhukumu Bi Justina Malela alipompata na hatia ya kupokea pesa hizo kutoka kwa Bi Naomi Musyoka kumsaidia kupata cheti cha kuzaliwa cha mtoto.

Bw Ogoti alisema upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi uliothibitisha kuwa Bi Mulela alipokea mlungula huo kumtengenezea Bi Musyoka cheti cha kuzaliwa cha mtoto alichokuwa amekiytafuta kwa udi na uvumba bila mafanikio.

“Mlalamishi alitaka kumchukulia mpwawe cheti cha kuzaliwa lakini hakujua utaratibu wa kufuata akipata licha ya kukisaka kwa muda bila ufanisi,” mahakama ilisema.

Bi Musyoka, 26 alieleza mahakama kuwa alijulishwa Bi Mulele na afisa anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserikali linalohudumia watoto Bw Bernard Lutta katika eneo hilo la Kibera..

Mlalamishi alisema mnamo Septemba 8, 2016 aliwasiliana na mshtakiwa kwa kumpigia simu. Walielewana jinsi atatengenezewa cheti cha kuzaliwa.

Korti ilisema mshtakiwa aliitisha Sh3,000 lakini baada ya Bi Musyoka kujitetea walisikizana amtumie kwa njia ya M-pesa Sh2,500.

Mshtakiwa hakumpelekea cheti hicho siku hiyo kisha akafunga simu. Ilibidi Bi Musyoka atembelee afisi ya Bi Mulela na pia mshtakiwa hakutaka kumwona.

Mlalamishi alisababisha kioja katika afisi ya hiyo ya kutoa huduma. Bi Ogoti alimpata na hatia mshtakiwa na kusema ujumbe wa M-Pesa ni ushahidi wa kutosha mshtakiwa alidai hongo hiyo.

Akijitetea Bi Mulela alisema yuko na watoto wawili na hana mume na kuisihi korti iamuru atumikie kifungo cha nje. Pia aliomba msamaha akisema anajutia matendo yake.

“Ulimnyanyasa mwananchi badala ya kumsaidia. Hili ni kosa mbaya. Umepatikana na hatia. Utalipa faini ya Sh500,000 ama kifungo cha miaka miwili gerezani,” aliamuru Bw Ogoti na kumuruhusu mshtakiwa akate rufaa katika muda wa siku 14.

 

  • Tags

You can share this post!

Mapato kutoka kwa Wakenya walio ughaibuni yaongezeka

Mshukiwa wa wizi wa mamilioni atokwa na jasho ajabu...

adminleo