Habari Mseto

Familia 1,000 zaachwa bila makao Turkana

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY LUTTA

Zaidi ya familia 1,000 zinazoishi karibu na Ziwa Turkana zimebaki bila makao baada ya maji ya ziwa hilo kuvunja kingo zake kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha humu nchini na nchi jirani ya Ethiopia.

Gavana wa Turkana Josphat Nanok alithibitisha kwamba ziwa hilo limepita kiwango chake kutoka mita 500 hadi 800.

“Maji hayo tayari yamefunika  hoteli na nyumba, na familia 1000 zimeachwa bila makao,” alisema Bw Nanok.

Alisema kwamba ziwa hilo lina  mamba na viboko ambao ni hatari kwa wakazi. Huku akiwaomba wakazi wahamie mahala salama, alisema kwamba watu wengi wamebaki  bila kazi kwani kazi ya uvuvi imeathirika.

Hoteli nyingi zimefunikwa huku wavuvi na wakazi wanaoishi karibu na ziwa hilo wakipoteza  kazi. “Madhara hayo tayari yameathiri sana Turkana Kaskazini na Turkana ya Kati,” alisema Bw Nanok.

Mbunge wa Turkana Kaskazini Christopher Nakuleu alisema kwamba hali hiyo isiyo ya  kawaida  inatokana na mafuriko ya mvua kubwa inayonyesha Ethiopia Kusini.

Alisema kwamba kumekuwa na mafuriko mengi kutoka mto Omo ambao ni chanzo kuu cha maji ya ziwa hilo.

 

TAFSIRI: FAUSTINE NGILA