• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Familia 2,600 kufurushwa Mukuru-Mariguini kupisha ujenzi wa Nyumba Nafuu

Familia 2,600 kufurushwa Mukuru-Mariguini kupisha ujenzi wa Nyumba Nafuu

NA SAMMY KIMATU

FAMILIA 2,600 katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Mariguini katika tarafa ya South ‘B’, kaunti ndogo ya Starehe zitalazimika kuondoka makao yao ili kupisha serikali kujenga nyumba za bei nafuu.

Akiongea katika mkutano wa kuhamasisha wakazi wa mtaa huo na washikadau wote, naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Starehe, Bw John Kisang alisema hata hivyo, waathiriwa wataondoka wakipewa kiinua mgongo na serikali kuwawezesha kuondoa mali yao.

“Furaha kwa wakazi wa mtaa huu ni kwamba serikali itawapatia hela kiasi ili kuwawezesha kuhamisha bidhaa zenu,” Bw Kisang akasema.

Mkuu huyo wa Starehe aliongeza kwamba serikali imepanga utaratibu wa kuwaondoa wakazi akisisisitiza zoezi hilo litafanywa kiutu.

Wakati huo huo, Bw Kisang amewaomba wakazi kukaa kwa amani hasa kati ya wamiliki wa nyumba na wapangaji akiwarai wapangaji kuendelea kulipa kodi ya nyumba hadi pale serikali itakapotoa mwelekeo watu wahame.

“Mpaka pale serikali itawaambia muanze kuondoka kutoka kwa nyumba zenu, endeleeni kulipa kodi ya nyumba hadi pale mtakapopewa ilani ya kuondoka,” Bw Kisang akasema.

Waliokuwa katika mkutano huo ni pamoja na katibu katika wizara ya Nyumba, Bw Hiran Kairo, Mkurugezi wa Idara ya Nyumba, Bi Mary Ndung’u waliosema mtaa huo utajengwa nyumba 3,400.

Bw Kisang alisema mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika mtaa huo ungekamilika mwaka 2018 lakini watu wachache walioupinga walipeleka kesi kortini.

Korti iliamua katika kesi hiyo kwamba mahali mtaa wa Mukuru-Mariguini umesimama ni katika ardhi ya serikali ndiposa serikali inatwaa shamba hilo na kuendelea na mpango wake wa kujenga nyumba zitazowafaidi wakazi wa Mukuru-Mariguini.

Vilevile, Bw Kisang asema awali, mtaa huo ulidaiwa kuwa katika ardhi ya mtu binafsi ambapo kufuatia ardhi hiyo kuzozaniwa mwaka 2014, watu wasiojulikana waliteketeza nyumba za watu wakitumia petroli.

“Ilikuwa ni majonzi wahalifu wasiojulikana kuvamia mtaa wa Mariguini na kunyunyizia makao ya watu petroli kabla ya kuwasha moto.

Hasara kubwa ilipatikana mwaka huo kwa sababu ya kupigania shamba la serikali,” Bw Kisang akafoka.

Alionya yeyote atakayethubutu kuhusika kwa njia moja au nyingine kuvuruga amani kwamba atakabiliwa sawasawa na mkono mrefu wa serikali na kwa vyovyote vile kushughulikiwa ipasavyo kisheria,” Bw Kisang akaonya.

Mkutano huo ulifanyika katika uga wa ofisi ya mwakilishi wa wadi ya Nairobi Kusini, Bi Waithera Chege katika mtaa wa Plainsview.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Tamko la Rais litaua motisha wa madaktari hata wakirudi...

Ruto kutafuta mtu mwingine baada ya Kemosi kukataa kazi ya...

T L