Familia ilipoyoteza watu 5 Solai, tena yapoteza mwingine Mai Mahiu
NA ERIC MATARA
FAMILIA moja Nakuru iliyopoteza watu watano kwenye mkasa wa bwawa la Solai mnamo 2018 ni miongoni mwa zile ambazo jamaa zao hawajulikani waliko kutokana na mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 52 katika eneo la Mai Mahiu, Jumatatu.
Familia ya Cate Wanderi sasa haijui hatima ya Isaac Thuku.
Bi Cate aliambia Taifa Leo katika mahojiano kwamba amejawa hofu kwani hana uhakika ikiwa mjukuu wake wa umri miaka mitatu yuko salama au la.
“Kwa familia yetu, mkasa huu umefungua majeraha ya mkasa wa bwawa la Solai ambapo tulipoteza wanafamilia watano. Tumehuzunika na hatujui la kufanya,” Bi Cate alisema.
Mvulana huyo alisombwa na mafuriko hayo akiwa pamoja na wazazi wake.
“Kwa bahati nzuri, wazazi wa Isaac waliokolewa lakini hatujui ikiwa Isaac yuko salama au la. Babake alijaribu kumwokoa lakini akateleza na kusombwa na maji. Bado hatujabaini ikiwa alifariki au aliokolewa,” akafichua Bi Cate.
Mbali na hayo, alisema kuwa wametembea katika baadhi ya vyumba vya kuhifadhi maiti na hospitali lakini mvulana huyo bado hajapatikana.
“Kwa siku nne sasa tumekuwa tukitarajia kumpata mtoto wetu lakini juhudi zote zimeambulia patupu, sasa tumeyaacha yote mikononi kwa Mungu.”
Kwa familia hiyo, mkasa wa Mai Mahiu umetonesha ‘kidonda’ kilichosababishwa na maafa ya Solai ya Mei 8, 2018, ambayo pia yaliua watu 48 na kuwasababishia ulemavu mamia ya wengine.
Bwawa la kibinafsi, lililo ndani ya Shamba la Patel Solai linalomilikiwa na kusimamiwa na Perry Mansukh Kansagara na Vinoj Jaya Kumar, lilivunja kingo zake usiku huo, na kuangamiza watu na kuharibu mali yao.