Familia ya Sharon yahitaji Sh1.3m kugharamia mazishi
Na RUTH MBULA
FAMILIA ya marehemu Sharon Otieno, ambaye alikuwa mpenzi mjamzito wa Gavana wa Migori Okoth Obado, inahitaji angalau Sh1.3 milioni kugharamia mazishi yake. Bw Douglas Otieno ambaye ni babake, alisema kamati ya mazishi iliyoundwa Jumapili ilitoa bajeti hiyo baada ya mashauriano ya kina.
Fedha hizo zitatumiwa kugharimia ada za mochari ambako mwili wake umekuwa umehifadhiwa kwa muda mrefu, kununua jeneza, gharama za usafiri na kuhudumia idadi kubwa ya waombolezaji wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi hayo.
Mwili wa marehemu umekuwa umehifadhiwa katika mochari iliyo Hospitali ya Med25 International katika eneobunge la Mbita, baada ya kuhamishwa kutoka hospitali ya Rachuonyo Level Four iliyo Oyugis kufuatia hofu za kiusalama.
Wakati huo huo, tarehe ya mazishi imesongezwa kutoka Oktoba 18 hadi 19.
Punde baada ya kuuawa kwa Bi Otieno, familia yake iliapa kwamba hatazikwa hadi wauaji wake waadhibiwe, lakini sasa wamesema wameridhishwa na jinsi washukiwa wakuu walivyokamatwa na kesi inavyoendelea kortini.
Mwenyekiti wa kamati ya mazishi, Bw Elijah Opiyo, alisema Bi Otieno ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Rongo, kaunti ya Migori, anastahili mazishi ya taadhima.
“Tunatarajia idadi kubwa ya waombolezaji ndiposa tunatoa wito kwa wahisani wachangie,” akasema.
Bw Samuel Onyango, ambaye ni babu wa marehemu, aliomba kuwe na amani wakati wa mazishi hayo.
Kwa upande mwingine, mamake, Bi Melida Auma, alisema mazishi hayo yasitazamwe kama kikomo cha upelelezi kuhusu kesi inayoendelea.
Alisema bado wana hofu kwani baadhi ya washukiwa hawajakamatwa akatoa wito kwa wapelelezi kuzidisha msako wao ili wauaji wote wakamatwe na kuadhibiwa.