Habari Mseto

Familia ya Sharon yataka haki itendeke

September 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

By Ruth Mbula

Miaka miwili sasa imepita tangu aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno kuuawa kinyama na kutupwa kichakani eneo la Oyugis, Kaunti ya Homabay waliomuua bado wakitembea huru bila kukamatwa.

Familia yake sasa inataka haki itendeke, ikisema kifo hicho kiliiletea huzuni nyingi, na wahusika wakuu bado hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Bi Sharon alikuwa ametoweka kwa muda wakati mwili wake ulipatikana Septemba 4, 2018.

Mshukiwa mkuu wa kifo cha Sharon ni gavana wa Migori Okoth Obado ambaye alikuwa mpenzi wake na baba wa mtoto aliyeuliwa akiwa tumboni baada ya kudingwa kisu mara saba.

Babaye Sharon Bw Douglas Otieno alisema kwamba kesi hiyo ilisimama wakati kuliripotiwa virusi vya corona nchini Mechi.

“Hatujasikia lolote kuhusu kesi hiyo. Tulikuwa tuende kusikizwa kwa kesi hiyo lakini hakuna chochote tumeambiwa,” alisema.

Waliomba korti iharakishe kusikizwa kwa kesi hiyo.

“Tunaomba haki itendeke kwa haraka kwasababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuondoa uchungu wa kumpoteza mtoto wetu wa kwanza,” alisema Bw Otieno.

“Tunaona kesi zingine zikiendelea, iko wapi kesi ya mtoto wetu? Kile tunataka ni haki kwa Sharon na mtoto wake,” alisema Bi Melida Auma, mamaye Sharon.

 

Tafsiri: Faustine Ngila