Familia ya Sharon yataka haki itendeke haraka
Na Ruth Mbula
Miaka miwili sasa imepita tangu aliyekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno kuuawa kinyama na kutupwa kichakani Oyugis kaunti ya Homabay lakini bado wauaji hawajakamatwa.
Bi Sharon alikuwa amepotea kwa muda wakati mwili wake ulipatikana Septemba 4, 2018.
Huku familia yake ikiathimisha miaka miwili baada ya kifo chake Ijumaa, ilisema kwamba kifo cha Sharon kilileta huzuni mwingi.
Mshukiwa mkuu wa kifo cha Sharon ni gavana wa Migori Okoth Obado ambaye alikuwa mpenzi wake na baba wa mtoto aliyeuawa akiwa tumboni mwa Sharon.
Bw Otieno alisema kwamba kesi hiyo ilisimama wakati kuliripotiwa virusi vya corona humu nchini mwezi Machi.
“Hatujasikia lolote kuhusu kesi hiyo. Tulikuwa tuende kusikizwa kwa kesi hiyo kabla ya jaribio lakini hakuna chochote tumeambiwa,” alisema.
Waliomba korti iharakishe kusikizwa kwa kesi hiyo. “Tunaomba haki itendeke kwa haraka kwasababu ndiyo njia peekee ya kuondoa uchungu wa kumpoteza mtoto wetu wa kwanza,” alisema Bw Otieno.
“Tunaona kesi zingine zikiendelea, iko wapi kesi ya mtoto wetu? Kile tunataka ni haki kwa Sharon na mtoto wake,” alisema Bi Auma.