• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Familia yaomba isaidiwe kupata maiti ya shujaa Dedan Kimathi

Familia yaomba isaidiwe kupata maiti ya shujaa Dedan Kimathi

Na Reginah Kinogu

FAMILIA ya Mpiganiaji wa Uhuru Dedan Kimathi imeiomba serikali kuisadia kupata mwili wa shujaa huyo ili wamwaandalie mazishi ya heshima.

Wakizungumza wakati wa ibada ya maombi ya kumuenzi katika eneo la Kahiga-Ini, Kaunti ya Nyeri, bintiye marehemu Bw Kimathi, Everlyne Kimathi alisema juhudi zao za kusaka mwili huo kwa muda wa miaka 15 hazijafua dafu hata baada ya kuelekezwa kwamba ulizikwa katika kaburi la pamoja ndani ya gereza la Kamiti.

“Tulianza kusaka alikozikwa na sasa imetuchukua miaka 15 lakini tuna imani kwamba tutaupata mwili wake hivi karibuni. Tulikuwa katika gereza la Kamiti mwaka wa 2017 na 2018 na kuonyeshwa mahali alikozikwa,” akasema Bi Kimathi.

Wakati uo huo, serikali ya Kaunti ya Nyeri imetenga Sh8milioni kuimarisha mwonekano wa eneo ambalo shujaa huyo alipigwa risasi ili kuwavutia watalii.

Waziri wa Utalii wa kaunti hiyo Diana Kendi alisema kwamba eneo hilo la kihistoria litazingirwa kwa ua kisha nyumba itakayotumika na wageni kupumzika ijengwe kuanzia mwezi ujao.

“Kila mara huwa tuna wageni wanaotembelea eneo hilo lakini wanakosa pa kutulia kutokana na makali ya jua na wakati mwingine hulazimika kupumzika chini ya mti. Tutajenga nyumba na vyoo ili kuhakikisha wageni wetu wanastarehe bila shida yoyote,” akasema Bi Kendi.

Kulingana na Bi Kendi, kaunti ya Nyeri imeandaa hafla ya maadhimisho ya siku ambayo Bw Kimathi aliuawa kwa kupigwa risasi katika uwanja wa Dedan Kimathi mjini Nyeri.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwaleta pamoja wapiganiaji wa uhuru kutoka maeneo mengine nchini ili kuondoa dhana kuwa ni Mau Mau pekee ndio walipigania uhuru wa taifa hili.

 

You can share this post!

Serikali yaondoa hofu kuhusu ‘Huduma Namba’

Mimi si mwandani wa Ruto – Oparanya

adminleo