• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Family Bank yaondolewa lawama kwenye kashfa ya NYS

Family Bank yaondolewa lawama kwenye kashfa ya NYS

Na RICHARD MUNGUTI

BENKI ya Family  (FBL) imeondolewa lawama katika kashfa ya Sh1.6 bilioni za shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) baada ya kusuluhisha kesi iliyoshtakiwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji.

Benki hiyo iliondolewa lawama baada ya kutimiza masharti kwamba ilipe faini ya Sh64.5 ambapo Sh24,500,000 zitapewa NYS na Sh40milioni wizara ya utumishi wa umma , spoti na utamaduni.

Benki hiyo ilikabiliwa na mashtaka sita ya kutoripoti utoaji pesa wa mmoja wa washukiwa wakuu katika kashfa ya NYS Bi Josephine Kabura.

Mahakama ilidaiwa ilikaidi sheria kwa kutoripoti kwamba mshukiwa huyo alikuwa anatoa pesa zinazozidi kiwango cha Sh1milioni.

Hakimu mkuu Francis Andayi alikubalia ombi la FBL na kukubalia suluhu kati yake na DPP na kuondoa jina la benki hiyo katika cheti cha mashtaka.

Tangu mwaka wa  2016 benki hiyo imekuwa ikichunguzwa kubaini kuhusika kwake katika kashfa hiyo ya NYS.

Katika taarifa Jumatano FBL kupitia kwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Dkt Wilfred Kiboro , benki ilisema ni kutokana na kujitolea kwake kikamilifu na kutii sheria ndipo imejitolea kupambana na ufisadi kwa udi na ufumba.

Dkt Kiboro alisema benki hiyo iliamua kuchukua hatua ya kusuluhisha kesi hiyo kwa kulipa faini ya Sh64.5milioni kwa nia ya kuhakikisha haki imetendeka katika muda uliofaa.

“Tunaamini hatua hii itaridhisha wanahisa na umma kwa jumla,” amesema Dkt Kiboro.

Mawakili Waweru Gatonye na Cecil Miller waliambia mahakama benki hiyo imetimiza masharti yote benki iliyoafikiana na DPP.

Naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Dorcus Oduor alimweleza Bw Andayi hapingi jina la FBL likiondolewa katika cheti cha mashtaka ndipo iondolewe lawama.

“Sipingi kesi hii dhidi ya FBL ikisahihishwa kuwa imetatuliwa na kufutiliwa mbali,” alisema Bi Oduor.

Huku kesi hiyo ikiondolewa benki hii imesema mikakati imewekwa ya kutathimini utenda kazi wake na usimamizi thabiti.

Maafisa wakuu wa benki hii wamesema watafuata sheria na kuwasiliana na benki kuu ya kenya (CBK) mara kwa mara sawia na wateja wake.

“Benki hii imeekeza katika kikamilifu kuhakikisha mitambo imewekwa kuthibiti ufisadi wa kifedha n ahata kuimbua mwongozo wa jua mteja wake (KYC),” alisema Dkt Kiboro.

Benki hiyo imesema imeanzisha mtaala wa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake wote kuhakikisgha wako sambamba na sheria mpya katika sekta ya benki.

You can share this post!

SHANGAZI: Akiwa mbali natamani burudani, akikaribia simtaki

KCB yatoa Sh75 milioni kufadhili mbio za magari

adminleo