Habari Mseto

Faraja kwa aliyejaribu kutorosha bintiye hospitalini KNH

February 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na Richard Munguti

BALAA iligeuka baraka kwa baba aliyejaribu kumtorosha bintiye kutoka Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) baada ya kushindwa kulipa bili ya matibabu ya Sh56,937.

Hii ni baada ya wahisani kujitokeza kumsaidia Boniface Murage Wangechi ambaye kisa chake kilipeperushwa na tovuti za kampuni ya Nation Media Group hapo Jumatatu.

Bw Murage aliamua kumtorosha mwanawe akiwa ndani ya mfuko wa kubebea mizigo kutoka KNH aliposhindwa kupata pesa za kulipa bili. Alikamatwa na walinzi wa KNH akitoka kwenye lifti na walipokagua mkoba wake wakapata alikuwa amebeba mtoto.

Kisa hiki kimedhihirisha jinsi gharama ya juu ya matibabu na ukosefu wa mfumo bora wa afya nchini unavyotatiza familia nyingi hasa za tabaka la chini.

Mfuko aliotumia kutoroshea bintiye uliwasilishwa mahakamani kama ushahidi. Picha/ Richard Munguti

Kundi la Sonko Rescue Team lililipa bili hiyo mnamo Jumatatu jioni na kufanikiwa kumtoa mkewe na mwanawe hospitalini na kuwanunulia vyakula na malazi. Hapo jana Gavana Mike Sonko alisema Bw Murage ataajiriwa kazi na serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Hapo jana pia, mmoja wa maafisa wa polisi waliohusika katika uokoaji katika shambulizi la hoteli ya Dusit D2 mwezi jana, Inspekta Emmanuel Tamooh, akimkabidhi baba huyo wa miaka 22 kitita cha Sh56,000 kusaidia familia yake.

“Nimetoa fedha kidogo kutoka kwa akiba yangu nimsaidie Bw Murage na familia yake,” akasema Bw Tammoh.

Alipofikishwa mahakamani jana, Bw Murage aliomba msamaha na kumweleza hakimu mkazi Bi Caroline Muthoni Nzibe kwamba anajuta kwa matendo yake.

“Ijapokuwa bili imelipwa, ulikuwa umetenda uhalifu na kwa hivyo mahakama imekuhukumu kifungo cha nje cha miezi mitatu,” Bi Nzibe aliamuru.

Bw Murage akiwa kizimbani. Picha/ Richard Munguti

Alimtaka mshtakiwa katika kipindi cha miezi mitatu asifanye kosa lolote na endapo atajihusisha na uhalifu na kurudishwa kortini atapewa kifungo kikali.

Baada ya uamuzi huo, mshtakiwa alitolewa korokoroni na kulakiwa na watu wa familia yake na kundi la Sonko Rescue Team lililompeleka nyumbani kwake Ongata Ngong kwa msafara wa magari kadhaa, ambako alipokelewa kwa shangwe na wakazi

Bintiye Murage alikuwa amelazwa katika hospitali ya KNH kati ya Januari 26 na Februari 16, 2019. Mtoto huyo alikuwa amezuiliwa hospitalini kwa siku sita ndipo babake akaamua kutumia mbinu zozote kumtoa bintiye hospitali alipokosa pesa.