Fowadi wa Arsenal mashakani baada ya jibwa lake kumng’ata kocha
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI wa Arsenal, Reiss Nelson, ameshtakiwa na kocha wake binafsi wa viungo anayedai kwamba jibwa la Kiitaliano linalomilikiwa na mchezaji huyo liliwahi kumng’ata wakipiga nalo picha ya ‘selfie’.
Saeid Motaali, 50, anadai jibwa hilo lililenga kumng’ata shingoni lilimuuma mkono ambao aliunyanyua akijaribu kujikinga akiwa kwenye bustani ya Nelson Kaskazini mwa jiji la London, Uingereza.
Inasemekana tukio hilo ilitokea mwaka wa 2020 baada ya Bw Motaali kumaliza kumfanyia Nelson masaji na kuomba wapige picha ya pamoja wakiwa na jibwa.
Kulingana na gazeti la Evening Standard nchini Uingereza, wanasheria wa Bw Motaali walisema: “Mbwa huyo alikuwa mnyama mkubwa mwenye nguvu na alionekana akiwa hatari kwa usalama.”
Madai ya Mahakama Kuu ya Uingereza yanamtuhumu Nelson kwa kushindwa kumdhibiti mbwa huyo ambaye alifunzwa mahsusi awe mlinzi.
Bw Motaali anasema hajawahi kuwezeshwa tena kufanya kazi kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita kutokana na tukio hilo la kung’atwa na jibwa.
Hapo awali, Nelson alikanusha mashtaka yote dhidi yake. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amepangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal mara moja pekee kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.
Itahitaji mafowadi tegemeo Bukayo Saka, Leandro Trossard au Gabriel Martinelli kupata jeraha ndipo naye apate nafasi katika kikosi cha kwanza cha Arsenal wanaonolewa na Mikel Arteta.