Habari Mseto

Gachagua afichua alikuwa msituni kwa maombi siku saba

May 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua mnamo Jumanne alifichua kwamba alikuwa amehamia ndani ya msitu wa Mlima Kenya kwa siku saba na kufunga kula na kunywa huku akiombea wenyeji wa Mlima Kenya.

Akiongea katika eneobunge la Gichugu katika Kaunti ya Kirinyaga alikohudhuria mazishi ya mwalimu Julius Kano Ndumbi, Bw Gachagua alisema ndani ya siku hizo saba, hakuwa na simu na hakuna mtu angemfikia akiwa ndani ya msitu huo.

“Ulikuwa wakati wa kutafakari, kuwazia na kuombea watu wetu wa Mlima Kenya wakumbatie umoja na wapendane kama ndugu,” akasema Bw Gachagua.

Alisema utengano uliopo Mlima Kenya unamkosesha usingizi na unamsumbua.

Alisema juhudi zake za kuombea Mlima Kenya uungane na uwe ukiongea kwa sauti moja hazitamfungia yeyote nje.

“Nitahakikisha kwamba wote wanaoongea kwa sauti moja. Sitamwacha yeyote nje kwa kuwa sisi ni watoto wa uzao mmoja wa Gikuyu na Mumbi,” akasema.

Bw Gachagua aliteta kwamba juhudi zake za kuunganisha jamii za Mlima Kenya zinapigwa jeki na heri njema za wenyeji na kamwe hatawatelekeza kama kinara na mfalme wao wa kisiasa.