Gaidi aliyeuawa Kwale alihusika katika uvamizi Dusit – Polisi
Na ALLAN OLINGO
UCHUNGUZI wa polisi umebaini kuwa mshukiwa wa ugaidi anayedaiwa kuongoza shambulizi katika jumba la Dusit jijini Nairobi, Mahir Riziki alikuwa akishirikiana na kiongozi wa genge hatari la Ngombeni Mohamed Rashid Mwatsumiro maarufu kama Modi ambaye alipigwa risasi na kuuawa mwezi uliopita.
Bw Modi aliuawa kwenye kisa cha ufyatulianaji wa risasi kati yake na kikosi hatari cha polisi wa kitengo cha Recce ambao walivamia makazi yake eneo la Ngomeni, Kaunti ya Kwale.
Wakati wa uvamizi huo, mmoja wa afisa wa polisi kutoka kitengo hicho, Jeremiah Mula alipigwa risasi tumboni na tayari amesafirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi kupokea matibabu maalum. Baada ya kumuua Bw Modi, polisi walipata bastola iliyokuwa na risasi 10, vilipuzi na nyaya za umeme.
“Stakabadhi iliyokuwa na jina la mshukiwa huyo wa ugaidi, ambaye kesi yake imekuwa ikiendelea katika mahakama ya Mombasa, ilipatikana. Vilevile vitabu ambavyo vilikuwa na maelezo kuhusu mafunzo ya dini ya Kiislamu pia vilipatikana,” ikasema ripoti ya polisi.
Kulingana na taarifa za polisi, Mabw Modi na Riziki waliondoka nchini na kusafiri hadi Somalia wakiwa na lengo la kujiunga na kundi la kigaidi la Al Shabab mnamo 2014 kisha wakarejea kimya kimya mwaka jana.
Washukiwa hao wa ugaidi wanadaiwa kuondoka nchini 2014 punde tu baada ya kuvamiwa kwa msikiti wa Masjid Musa ambao ulidaiwa kuwa eneo la kutolewa kwa mafunzo yenye itikadi kali.
Waliokuwa Maimamu wa msikiti huo Sheik Aboud Rogo na Abubakar Sharif almaarufu makaburi walidaiwa kuyatoa mafunzo hayo kwa vijana na pia kuwasajili kuwa wanachama wa Al Shabab. Mabw Rogo na Makaburi waliuawa 2012 na 2014 mtawalia.
“Watu wengine waliosafiri hadi Somalia wakati huo walikuwa Ahmed Omar Said maarufu kama Dogo, Ramadhan Hamisi Kufungwa kwa jina la utani Rama, Mohamed Ebrahim kwa lakabu ya Daddy na Salim Ahmed Mohamed aliyejulikana kama Lascano,” ikasema ripoti ya polisi.
Maelezo zaidi ya ripoti hiyo yanafichua kwamba Modi aliunda mtandao wa genge hatari, wa kutoa mafunzo yenye itikadi kali eneo la Kwale baada ya kurejea nchini.
Bw Mahir naye kimya kimya aliendeleza mpango wa kuhakikishan uvamizi kwenye hoteli ya Dusit D2 unafanikiwa.