• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 3:36 PM
GALANA-KULALU: Maseneta waunga kaunti ihusishwe

GALANA-KULALU: Maseneta waunga kaunti ihusishwe

Na PETER MBURU

GAVANA wa Kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amelaumu serikali kuu kwa kukosa kuhusisha serikali ya kaunti yake katika shughuli za utekelezaji wa mradi wa kilimo wa Galana- Kulalu, wakati maafisa katika Wizara ya Kilimo wanauharibu kwa tamaa zao za kupata pesa kutokana na mradi huo.

Bw Dhadho alilalamika kuwa kaunti yake imeachwa nje katika mradi mkubwa kiasi hicho, wakati wakazi wa kaunti yake ni baadhi ya Wakenya wengi ambao wamekuwa wakiathirika na ukame na njaa.

Gavana huyo alisema kuwa pamoja na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi wamekuwa wakitafuta kikao na Rais Uhuru Kenyatta kupaza sauti zao, akisema kuwa kuna washauri wa Rais ambao wanampotosha.

Bw Dhadho alikuwa akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Uhasibu alipofika mbele yake bungeni jana.

“Tunataka kuhusishwa katika kamati ya utekelezaji wa mradi huo kwani baadhi ya wanaohusika wamekuwa wakifanya mambo yao ili kupata pesa, hali ambayo imesababisha mradi huo kukosa kuzaa matunda,” gavana huyo akasema.

Alisema kuwa baadhi ya watu wanaohusika na utekelezaji wa mradi huo waliondoa mipango iliyokuwako awali ili wapate pesa, suala ambalo liliwafanya maseneta kuingilia na kusema kuwa sharti kaunti hiyo ipewe fursa kuhusika katika utekelezaji wa mradi huo.

“Kilimo ni suala la ugatuzi na hivyo ni sharti kaunti ihusishwe, ni kwa kuhusishwa tu ndipo mtaweza kuhakikisha kuwa mambo yanaendeshwa inavyofaa na kulalamika yanapoenda kombo,” seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi akasema.

Mradi huo wa Galana Kulalu ulianzishwa mnamo 2013 na serikali kuu, tangu wakati huo mabilioni ya pesa yakimwagwa ndani yake na serikali miaka ya fedha iliyofuata, japo hakuna matunda yoyote yameonekana miaka sita baadaye.

Mpango ulikuwa kufanya kilimo cha unyunyiziaji maji katika shamba la ukubwa wa ekari milioni 1.7, ambacho kingezalisha chakula cha kutosha kulisha Kenya.

Hata hivyo, hadi leo, mradi huo haujafanikiwa ila umekuwa hasara tupu, mabilioni ya pesa za mlipa ushuru yakipotelea ndani, na madai ya ufisadi ndani yake yakizidi kuibuka.

Kaunti za Kilifi na Tana River zimekuwa zikipigania kupokezwa usimamizi wa mradi huo, japo wizara ya kilimo nayo imekuwa ikijitetea kila mara kuwa inauendesha vyema, licha ya hasara za wazi zinazoonekana.

“Hatuwezi kuruhusu serikali kuleta watu kwa kuwa inawaita wataalam kutoka Israel ama katika maafisi Nairobi na kupuuza wakulima wa eneo hilo ambao ndio wanafahamu jinsi wamekuwa wakifanya kilimo miaka yote. Sharti kaunti zihusishwe,” seneta wa Homa Bay Otieno Kajwang akasema.

You can share this post!

Breki kwa marufuku ya matangazo ya kamari

NASAHA: Ramadhani ni fursa ya kuzitakasa nafsi zetu na...

adminleo