Gavana ahimiza ubunifu utumike kunoa vipaji
NA SAMMY WAWERU
Janga la Covid-19 limedhihirisha Kenya ina uwezo kujitengenezea nyingi ya bidhaa badala ya kutegemea mataifa ya kigeni ilhali ina malighafi na raslimali za kutosha.
Gavana wa Isiolo, Mohamed Kuti alisema Jumatatu kwamba ubunifu ulioonyeshwa na baadhi ya Wakenya kipindi hiki cha corona ni ishara kuwa taifa hili linaweza kujiimarisha katika sekta ya viwanda.
Akitumia mfano wa maski na vitanda kulaza na kutengea wagonjwa wa virusi vya corona, vifaa ambavyo kwa sasa vinaundiwa humu nchini, Bw Kuti alisema ni dhihirisho Kenya ina vipaji wenye uwezo kuimarisha sekta ya viwanda.
Bw Kuti ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Baraza la Magavana Nchini (CoG), alisema hayo katika kongamano la Covid-19 lililoandaliwa katika Ukumbi wa Kitaifa wa Mikutano, KICC, jijini Nairobi.
“Wakati nilipoingia kwenye ukumbi huu nilikagua baadhi ya bidhaa zilizoko kwenye meza, kama vile vichokoneo vya meno na nyinginezo…nyingi ya bidhaa nilizotazama zimeundiwa nje ya nchi. Tunahitaji kuanza kujiundia bidhaa zetu wenyewe, tuna malighafi na raslimali za kutosha.
“Sioni haja ya bidhaa tulizo na uwezo, kutengenezewa nje ya nchi. Corona imedhihirisha tuna uwezo kujiundia bidhaa zetu wenyewe. Kwa mfano, kila kaunti kwa sasa inajitengenezea maski. Vitanda vya kulaza na kutenga wagonjwa wa Covid-19 vinatengenezwa na mafundi wetu, wa ndani kwa ndani,” akafafanua Gavana huyo.
Kutokana na mikakati iliyowekwa na serikali kupambana na janga la corona, ikiwemo kuimarisha viwanda hasa vya nguo na ambavyo vimechangia pakubwa kutengeneza maski, Bw Kuti alisema hatua hiyo imeonyesha sekta ya viwanda na Juakali zinaweza kupigwa jeki na kusaidia kutatua dondandugu la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
“Awali, tuliagiza vifaa vingi kutoka nje kukabili corona. Kwa sasa tunajiundia nyingi yavyo. Ni wazi tuna uwezo kuimarisha sekta ya viwanda na Juakali,” akasema.
Mbali na maski na vitanda vya wagonjwa, bidhaa zingine zinazosaidia kupambana na corona na vinavyotengenezewa nchini ni pamoja na sanitaiza, sabuni ya majimaji, kati ya nyinginezo.
Akitoa maoni kuhusu uimarishaji wa sekta ya viwanda katika kongamano hilo ambalo lilifunguliwa na kuhudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, Mwanasheria Mkuu, Profesa Paul Kihara alisema Wakenya wanapaswa kukumbatia matumizi ya bidhaa zilizohundiwa humu nchini, katika kile alitaja kama “kununua Kenya ili kuunda Kenya”.