Gavana akana madai hospitali haina vifaa vya kuthibiti corona
NA WAWERU WAIRIMU
Gavana wa Kaunti ya Isiolo Mohamed Kuti amewalaumu maadui wake wa kisiasa kwa kueneza uvumi kwamba chumba cha watu mahututi wa corona katika hospitali ya rufaa ya kaunti hiyo hakina vifaa vinavyohitajika.
Gavana huyo alisema kwamba vitanda sita vya ICU vinafanya na kamati ya maseneta iliyotembelea hospitali hiyo inanaeza kuthibitisha hayo.
“Tulitembeza kamati ya maseneta inayoshungulikia corona na wananchi waliokuwepo wakajionea kuwa ICU yetu inafanya kazi. Wananchi na Wakenya sasa wanajua nani aongea ukweli na wanaoongea propaganda ili kujitafuia umaarufu wa kisiasa,”alisema Dkt Kuti.
Alikana madai kwamba vitanda vingine vilikuwa vya kukodisha kutoka hospitali za kibinafsi akisema kwamba vilinunuliwa kutoka kwa Mission for Essential Drugs Supplies[MEDS] na wana stakabathi za kuthibitisha ununuzi.
Aliwakemea wanasiasa wanaoeneza uvumi kuwa ni aibu kuweka siasa kwenye maswala ya afya.
Gavana huyo alisema kwamba wamewafunza maafisa 1,470 wanaohusika na sekta ya afya na kuwapa barakoa 50,000, chakula na dawa kwa maeneo ya Iresaboru yalioathirika na mafuriko.