Gavana akutana na wahasiriwa wa ubomoaji soko Githurai
Na SAMMY WAWERU
IKIWA ni wiki mbili baada ya maduka na vibanda vya mamia ya wachuuzi wa bidhaa za kula na mazao ya kilimo kubomolewa Githurai, Gavana wa Kaunti ya Kiambu, James Nyoro alikutana nao na kuahidi kuwahamisha hadi katika soko jipya linaloendelea kutengenezwa pindi litakapokamilika.
Akizungumza baada ya kupokea malalamishi ya wafanyabiashara hao, Bw Nyoro alisema soko hilo la ghorofa litafunguliwa hivi karibuni.
“Utengenezaji wa soko la Githurai unaoendelea utakamilika hivi karibuni na mtahamishiwa humo,” Gavana akasema.
Alisema serikali ya kaunti ya Kiambu kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa inafanya kila iwezalo kuhakikisha hawatakosa mahala pa kuzimbulia riziki.
Mnamo Agosti 26, 2020, wachuuzi wa bidhaa za kula na mazao yakiwemo matunda, wanaouzia kandokando ya reli waliamkia kupata vibanda na maduka yao yamebomolewa na matingatinga.
Walikadiria hasara ya bidhaa za thamani kubwa. Siku moja baada ya tukio hilo, eneo la soko lililoathirika liliteketezwa kwa moto chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi ambao hawakuwa wamevalia sare.
Wachuuzi hao hata hivyo walisema hawakuwa wamekataa kuondoka, ila walichoomba ni wapewe muda wajiandae watakakoelekea kujiendeleza kimaisha.
“Hatukukataa kuondoka, tunachoomba ni watupe muda tujipange,” akasema James Gikundi, mmoja wa wafanyabiashara hao.
Licha ya kuahidiwa nafasi katika soko jipya, baadhi wanasema halitaweza kuwasitiri wote.
“Wachuuzi wote Githurai waliahidiwa soko hilo, ni muhimu tuambiane ukweli sote hatutatoshea humo. Serikali itutafutie ardhi nyingine,” akapendekeza mfanyabaishara mmoja.
Soko lililobomolewa linakadiriwa kuwa na zaidi ya wachuuzi 1,000.
Ubomoaji wa soko hilo ulitekelezwa na Shirika la Reli Nchini. Gavana Nyoro alisema ubomozi huo ulilenga kuruhusu ukarabati wa reli inayounganisha jiji la Nairobi, Thika na Nanyuki unaoendelea ili kufufua shughuli za usafiri na uchukuzi kwa njia ya garimoshi.
Wakati huohuo, gavana huyo alihimiza wafanyabiashara wa Githurai kuunda makundi ya ushirika, wayasajili na kuweka akiba ili waweze kupata mikopo kuimarisha kazi zao. Aidha, Bw Nyoro alitoa mchango wa Sh2.5 milioni kuanzisha mpango huo.