• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Gavana Muthomi Njuki atupwa ndani pamoja na mkewe

Gavana Muthomi Njuki atupwa ndani pamoja na mkewe

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya kuamua kesi za ufisadi Jumanne ilisikitishwa na tabia ya baadhi ya viongozi ya kushirikisha familia zao katika ufisadi na uporaji wa mali ya umma.

Hakimu mkuu Douglas Ogoti alisema katika siku za hivi punde viongozi wametiwa nguvuni na kushtakiwa pamoja watu wa familia zao kwa kushiriki visa vya ufisadi.

“Inasikitisha jinsi viongozi wanawashirikisha watu wa familia zao kushiriki uhalifu wa uporaji wa mali za umma huku baadhi yao wakiwa hawajui kilichofanyika na wanashtukia tu wamekamatwa na kushtakiwa mahakamani,” alisema Bw Ogoti.

Hivi majuzi, Gavana Okoth Obado wa Migoti alishtakiwa pamoja wanawe wanne kwa ufisadi wa Sh73m. Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mkewe Susan walishtakiwa katika kashfa ya zaidi ya Sh500m.

Familia ya Ngirita nayo imeshtakiwa katika kashfa ya NYS ya Sh790m na sasa Bw Njuki na mkewe na wakurugenzi wa kampuni ya Westomaxx Investments Limited (WIL) Kenneth Mucuiya na Caroline Sheila Wambui wameshtakiwa katika kashfa ya Sh34m.

Huku akisema nchi imeshika mkondo mbaya, Bw Ogoti alisema viongozi wamezindua humu nchini tabia ambayo jamii inasikitika.

Bw Ogoti amewashauri mawakili wasome Makala jinsi inavyotendeka viongozi wakishirikisha familia zao katika kutenda uhalifu.

Katika kesi ya kashfa ya Tharaka Nithi Bw Njuki na mkewe Margaret Muthoni Mugweru pamoja na wakurugenzi wa kampuni ya Westomaxx Investment Limited (WIL) Kenneth Mucuiya Ngai na mkewe Caroline Sheila Wambui na ajenti wao masuala ya fedha Japheth Muriithi Gitonga walishtakiwa katika kashfa hiyo ya Sh34.9m zilizoibwa kutoka kaunti ya Tharaka Nithi kati ya Januari 2018 na Oktoba 31 2018.

Bw Ogoti aliombwa na mawakili Paul Nyamondi na Muthomi Thiankolu wanaowakilisha Njuki na Muthoni na Mucuiya na Sheila na Gitonga awaachilie kwa dhamana sisizo vya viwango vya juu.

“Mzigo wote wa dhamana utabebwa na waume wa wake hawa pamoja na kampuni zao,” alisema Bw Thiankolu.

Hakimu alielezwa na Bw Thiankolu mkewe Kenneth amelazwa hospitali akiwa na changamoto ya kiafya.

“Dhamana ile utakayoipa familia hii itaathiri hata maisha ya mtoto wa siku saba aliyezaliwa kwa njia ya upasuaji,” akadokeza wakili.

Kiongozi wa mashtaka Bi Hellen Mwatellah (aliyesimama) alipoongoza mashtaka. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Alisema gharama ya hospitali na dhamana”zote zimo mabegani mwa Kenneth.”

“Naomba hii mahakama itilie maanani ni Mucuiya atakayebebeshwa mzigo wote wa dhamana na gharama nyinginezo.

Washtakiwa wote 18 waliomba waachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu ikitiliwa maanani makali ya Covid-19.

Kiongozi wa mashtaka Bi Hellen Mwatellah aliomba mahakama izingatie kiwango cha pesa kilichopotea.

“Naomba hii korti izingatie kwamba zaidi ya Sh34.9m zilipotea kwa njia ya undanganyifu na adhabu ni miaka 14 gerezani na faini isiyopungua Sh64milioni kwa vile ni kesi ya ufisadi na uzoroteshaji wa uchumi,” alisema Bi Mwatellah.

Bi Mwatellah aliomba mahakama izingatia athari zinazosababishwa na ufisadi kwa nchi.

Bw Ogoti ataamua Jumatano kiwango cha dhamana atakachowaachilia washtakiwa.

Bw Njuki pamoja na washtakiwa wote walikana mashtaka ya kula njama kuilaghai kaunti hiyo Sh34,998,500 katika ununuzi wa mtambo wa kuteketeza taka.

Kampuni ya Generation Electronic and Allied inayomilikiwa Gavana na mkewe Margaret na David Mbugua Mwangi imeshtakiwa kununua mtambo huo na kuukabidhi serikali ya kaunti ya Tharaka Nithi kisha ikadanganya ulinunuliwa na kampuni ya Westomaxx.

Malipo ya ununuzi na uwekaji wa mtambo huo yalipokewa na kampuni ya Westomax kupitia benki ya Consolidated Bank tawi la Embu.

Walioshtakiwa mbele ya Bw Ogoti ni Njuki, mkewe Margaret na kampuni yao Generation Electronic and Allied Limited, Fridah Muthoni Murungi, Floridah Kiende Ndwigah, Highton Muriithi Njue, Teresiah Kagoji Mburia, Lee Mwenda Munene, Japheth Mutungi Nkonge, Emily Nkatha Micheni, Mike Miandi Murithi, Elosy Karithi Matti, Mucuiya, Sheila, Allan Murithi Gitonga, Japheth Gitonga Nyange ,George Miano Mugweru, Genetech Supplies  Ltd na Kenstar Electrical and Hardware Ltd.

Washtakiwa wote 21 walikana shtaka la kula njama za kuifilisi serikali ya kaunti ya Tharaka Nithi Sh34,998,500 katika ununuzi na uwekaji wa mtambo wa kuteketeza takataka kati ya Januari 2018 na Oktoba 2018.

Gavana Njuki , mkewe Margaret Muthoni Mugweru, Mwangi na kampuni yao Generations Electronic walikana shtaka la kushiriki udanganyifu.

Wakili wa Gavana Muthomi Njuki, Bw Thiankolu na mawakili wengine waliowatetea washtakiwa. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Bw Njuki alikabiliwa na shtaka kuficha alikuwa mshirika wa biashara na kampuni iliyopewa zabuni ya kununua mtambo huo,

Fridah ambaye ni afisa mkuu wa wizara ya mazingira alishtakiwa kuidhinisha kinyume cha sheria malipo ya Sh34,998,500 kwa kampuni ya Westomaxx kwa ununuzi na uwekaji mtambo huo. Alikabiliwa na mashtaka matano.

Wakamati wa ukaguzi Mwenda, Mutugi, Nkatha, Mwiandi na Kariithi walishtakiwa kwa kukiuka sheria za ukaguzi na ununuzi wa mali ya kaunti hiyo.

Njue na Teresia ambao ni wakuu wa fedha walishtakiwa kwa kuidhinisha malipo ya mtambo huo kinyume cha sheria.

Mucuiya, Sheila, Gitonga na kampuni yao Westomaxx walishtakiwa kwa ubadhirifu wa pesa kwa kupokea zaidi ya Sh32m kutoka benki ya Consolidated wakijua hawakununulia kaunti ya Tharaka Nithi mtambo huo.

Washtakiwa watajua hatima yao ya dhamana Jumatano. Waliagizwa wazuiliwe katika vituo vya polisi vya Parklands, Kileleshwa na EACC.

Bw Ogoti alisema atakagua mashtaka ya kila mmoja kabla ya kuamua kiwango cha dhamana atakayowapa. Aliishutumu afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kwa kuchelewesha kuwasilisha kortini cheti cha mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Tafsiri ya Kiingereza ya ‘it doesn’t...

VITUKO: Pengo atua Migingo, kumbe tabasamu ya kike...