Gavana Nassir aajiri aliyekuwa mlinzi wa Raila kushauri kuhusu usalama
GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswammad Nassir, amemwajiri Bw Maurice Ogeta, aliyekuwa mlinzi wa kinara wa zamani wa ODM hayati Raila Odinga, kuwa mshauri wa masuala ya usalama katika kaunti hiyo.
Bw Nassir, ambaye pia ni naibu kinara wa ODM, alisema Bw Ogeta aliajiriwa kwa sababu ya tajriba yake ya masuala ya kiusalama.
Kwa takriban miaka 18, Bw Ogeta alikuwa mlinzi wa Bw Odinga, akimlinda katika vipindi hatari vya kisiasa, ikiwemo maandamano, misafara ya hatari na hata wakati ambapo joto la kisiasa nchini lilikuwa limepanda.
Alikuwa na Bw Odinga katika dakika zake za mwisho akipokea matibabu nchini India.
Wakati huo huo, Bw Nassir pia alitangaza amemwajiri Bw Ken Ambani kuwa mshauri wake wa masuala ya sanaa katika kaunti.
Bw Ambani ambaye pia ni mwigizaji tajika nchini, alihudumu kama waziri wa Huduma ya Umma, Jinsia, Vijana na Michezo katika kaunti hiyo hadi Julai 2025 kulipofanyika mabadiliko katika baraza la mawaziri.
“Ujuzi wake wa sekta ya sanaa utatusaidia tunapoweka juhudi za kufufua na kukuza sanaa bunifu Mombasa kwa manufaa ya wasanii, vijana na uchumi kwa jumla,” akaongeza Bw Nassir.
Alisema teuzi hizo ziliidhinishwa kisheria kupitia kwa Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti.