• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Gavana Nyong’o aondoka hospitalini

Gavana Nyong’o aondoka hospitalini

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kisumu Anyang’ Nyong’o Alhamisi aliruhusiwa kuondoka kutoka Hospitali ya Aga Khan, Nairobi ambako amekuwa akitibiwa kwa muda wa wiki moja baaDa ya kuugua.

Gavana Nyong’o aliugua mnamo Jumamosi alipokuwa akihudhuria hafla ya kutawazwa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Kisumu Kasisi Philip Anyolo.

Aliomba radhi kuondoka katika hafla hiyo ili aende atibiwe baada ya kuanza kuhisi maumivu. Alitibiwa katika hospitali ya Aga Khan Kisumu kwa saa kadha kabla ya kusafirishwa kwa ndege hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

Viongozi kadhaa wa kisiasa walimtembelea Profesa Nyong’o hospitalini mnamo Jumatano. Wa kwanza kuwasili alikuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Baadaye jioni, Naibu Rais William Ruto aliwasili hospitalini humo kumjulia hali. Aliandamana na mwenyekiti mpya wa baraza la magavana Wycliffe Oparanya na naibu wake Mwangi wa Iria.

Wengine walikuwa naibu Gavana wa Kisumu Dkt Mathew Owili na Mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi.

“Nimemtembelea Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o hospitalini. Nimefurahi kwamba anaendelea vizuri na ninamtakia afueni ya haraka,” Dkt Ruto akasema kwenye ujumbe wa twitter.

Kutokana na kuugua huko, Profesa Nyong’o alikosa kuhudhuria mkutano wa Baraza la Magavana (CoG) mnamo Jumatatu ambapo maafisa wake wapya walichaguliwa.

Nyong’o alikuwa mmoja wa magavana wanne waliowania wadhifa wa mwenyekiti wa baraza hilo ambapo Bw Oparanya alichaguliwa kuwa mwenyekiti.

Madaktari walisema kuwa Gavana Nyong’o “ameimarika kiafya”.

You can share this post!

Bandari yang’oa Mathare United kileleni

Uhuru ashangaza kuwaacha walinzi wake mataani

adminleo