Gavana Waititu aonya matapeli wanaohangaisha watumiaji wa soko Witeithie
Na LAWRENCE ONGARO
MAWAKALA ambao wamezoea kuhangaisha wakazi na watumiaji wa soko la Witeithie eneo la Juja, wamepigwa marufuku kuendesha shughuli zao huko.
Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu, amesema hataki kuwaona watu hao wakiendesha shughuli zozote katika soko hilo.
Akizungumza katika soko la Juja mnamo Alhamisi, Bw Waititu aliwataka wakazi wa Juja wajipange ili kuwachagua viongozi wapya watakaoendesha shughuli za kuendesha soko la Witethie.
“Nimepata ripoti kuwa kuna watu fulani ambao hujigamba kama ndiyo wenye soko huku wakiwauzia wakazi nafasi ya kufanyia biashara zao. Siwezi kubali tabia ya aina hiyo kuendelea,” alisema Bw Waititu.
Alisema hakuna mtu yeyote aliye na mamlaka kupokea fedha kutoka kwa wananchi kwa manufaa yake mwenyewe.
Bw Waititu aliyeandamana na naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Juja, Bw Charles Mureithi na wakuu wa usalama alisema hakuna mtu yeyote aliyepewa uwezo kupokea pesa kutoka kwa mwananchi kwa njia ya ulaghai.
“Nyingi wananchi msikubali kwa vyovyote kutoa pesa kwa walaghai wanaozunguka wakisanya pesa kwa manufaa yao wenyewe,” alisema Bw Waititu.
Alisema wananchi watafanya bahati na sibu ili kutafuta wale watapewa nafasi katika eneo la soko.
“Mpango huo unastahili kutekelezwa kwa njia ya uwazi bila kubagua yeyote. Yule atafanikiwa kupata itakuwa ni bahati yake,” alisema Bw Waititu.
Miradi
Alisema hospitali, shule ya msingi na vyoo vitajengwa eneo la Juja ili kutosheleza matakwa ya wingi wa watu walio eneo hilo.
Aidha, aliwataka wale wanaendesha biashara zao eneo la Witeithie wadumishe amani na wajiepushe na uhuni.
Naibu kamishna Bw Mureithi alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba hali ya usalama unaimarishwa kwa muda wa saa 24 huku polisi wakipiga doria kila sehemu.
Alisema kwa siku za hivi karibuni afisi yake imeweka usalama wa kutosha kwa kupambana na wahalifu ambao walikuwa wakisumbua wakazi wa Juja.
Aliwahimiza wakazi wa Juja kushirikiana na maafisa wa usalama ili kukabiliana na wahalifu hao.
Bw John Thungu, mkazi wa Juja aliipongeza idara ya usalama kwa kupambana na wahalifu wa eneo hilo.
” Siku hizi sisi wakazi wa Juja tuna amani na kwa hivyo tunapongeza maafisa wa usalama kwa kazi yao njema,” alisema Bw Thungu.