Habari Mseto

Genge la matineja lateka mji kwa uhalifu

December 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA STEPHEN ODUOR

GENGE la vijana wa chini ya miaka kumi na sita limeibua hofu miongoni mwa wakazi mjini Madogo, Kaunti ya Tana River kwa kushambulia kwa visu na silaha nyingine hatari.

Kundi hilo linalojiita Gaza sawa na jingine maarufu Nairobi, linashirikisha vijana zaidi ya kumi walioacha shule za upili na hata za msingi mjini Madogo.

Limeteka mji huo kwa fujo na kuufanya kuwa himaya yao.

Kwa muda wa miezi mitatu sasa, wakazi wa eneo hilo wamedhulumiwa. Wengi wao wanauguza majeraha ya visu, huku wengine wakilalamikia hasara ya mali ya thamani walizoibiwa katika maeneo ya biashara na nyumbani.

Anne Mukami anakumbuka jinsi alivyoibiwa pesa na vijana hao, pale alipokuwa ametoka katika pilkapilka za kuchuma mjini Garissa.

“Nilikuwa na kama Sh65,000 hivi, na nilikuwa nimepanga kulipia mali fulani keshoye. Sasa tuliposimama na mtu wa bodaboda dukani, walitokea vijana saba. Mmoja alikuwa na kitu kama bunduki kwa kiuno, hao wengine walikuwa na visu na mapanga makali wakaniambia niwape kila kitu mpaka leso na mtandio,” alisimulia. 

Hata baada ya kumuibia, vijana watatu kati yao waliabiri pikipiki aliyokuwa ameletwa kwayo baada ya kumpora hata dereva, huku wanne kati ya vijana wale wakimsindikiza Bi Mukami hadi mlangoni pake na kumuonya dhidi ya kuripoti kisa hicho kwa polisi, huku wakimwambia kuwa akithubutu, taarifa itawafikia hata kabla ya jua kuchomoza.

Walihakikisha ameingia kwake na wakampa onyo dhidi ya kupiga ukemi wa kuwaamsha majirani, la sivyo wangemchomea ndani ya nyumba.

Bi Mukami alimalizia uchungu wake kwa machozi ndani ya nyumba na kukata uamuzi wa kuuhama mji na kuelekea Garissa.

Asubuhi ile alipata taarifa kuwa aliyekuwa dereva wa pikipiki alivuliwa nguo na kuachwa uchi wa mnyama baada ya kutiwa alama za kisu, hata baada ya kuwafikisha walikokuwa wakienda, na baadaye kuambiwa asisimame popote isipokuwa kwake.

“Walimwambia kuwa tayari washamtia alama ya Gaza na kwamba hawatamwibia tena ila wakimhitaji kwa shughuli yoyote watatafuta huduma zake,” akasema.

Ilibainika kuwa baadhi ya waathiriwa wa genge hili walikuwa na alama za visu kwa mtindo fulani, huku wale wanaosumbua wanapoporwa hudungwa visu na kuachwa na majeraha mabaya.

Wanaotiwa alama hupewa onyo dhidi ya kuwaonyesha watu alama hizo, huku wakiwekwa chini ya ulinzi wa watu wasiowajua katika maeneo yao ya kazi.

Kwa mujibu wa wakazi, kadri siku zinavyopita, kundi hilo linazidi kuwa kubwa na jinamaizi hatari katika jamii, kwani, vijana tayari wanadondoka shuleni na kujipata katika makundi hayo.

Juhudi za kuwafikia maafisa wakuu wa polisi hazikufua dafu hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii. Baadhi ya maafisa hao akiwemo kamanda wa polisi katika kaunti walidinda kupokea simu wala kujibu jumbe kuhusiana na suala hilo.

Hata hivyo, duru zinazoaminika miongoni mwa polisi zilieleza Taifa Leo kuwa viajana watatu wanaoaminiwa kuwa wafuasi wa kundi hilo la Gaza na kutiwa mbaroni waliachiliwa.

Kwa vijana walio katika maeneo ya kazi haswa wanawake, hulazimishwa kutoa ada ya Sh1,000 kwa kundi hilo kila mwisho wa mwezi.

Ada hiyo huchukuliwa kwa ajili ya kuwalinda na kama Ishara ya kusalimu amri, la sivyo mtu hukosa amani kwa kuporwa na kupigwa kila siku na wakati mwingine kuibiwa kila kitu nyumbani.

Zainab Hawa amekuwa akilipa ada yake kila mwezi tangu anusurike kifo alipopiga ukemi katika pilkapilka za kuibiwa.

“Wao hugonga mlango hata saa nane usiku au waje katika maeneo yako ya kazi ama wakutane nawe kanisani. Hutajua iwapo wanakuja, na hutamjua ni nani kaja. Utasikia tu dogo flani kanisani hapo kando yako anakwambia ‘redeem bonga points’ ama ‘nipe sadaka ya mwezi’. Hapo ndipo utajua ni wao,” alisimulia.

Iwapo anayedaiwa hana pesa atembeapo, huambiwa azifikishe mahali fulani au labda kuziweka katika kituo fulani ambapo pindi zinapopokewa mambo hutulia.

Vijana hao hawapendi kutumia simu kuchukua ada, na huwa katili kwa yeyote anayekiuka ulipaji wa ada hiyo.

Wakazi sasa wanalazimika kuwa nyumbani kabla ya saa moja usiku ili kuepuka kukutana na vijana hao.

Kundi la Gaza lilisikika mwanzo mwezi uliopita, baada ya anayekisiwa kuwa kiongozi wao kutoa kanda ya video akijivunia wizi na shughuli zake za kikatili mjini Madogo na hata Nairobi.

Kijana huyo anayetambuliwa mjini kama Johnnie alitishia kuwaua watu watatu aliokisia walikuwa wakishirikiana na polisi katika ujasusi.

Wakazi wamewarai polisi kutumia mbinu zozote zile kumaliza uhalifu ambao sasa unaonekana kulemaza biashara mjini.