Ghadhabu baada ya Waethiopia kuua Wakenya 11 mkutanoni
Na CECIL ODONGO
VIONGOZI na wazee kutoka eneobunge la North Horr Kaunti ya Marsabit, walionyesha ghadhabu zao kufuatia mauaji ya watu 11 yaliyotekelezwa na jamii hasimu kutoka taifa jirani la Ethiopia Jumatatu.
Aliyekuwa Diwani wa Wadi ya Torbi, Yattani Wario, aliwaongoza wazee hao kukashifu mauaji hayo na kulaumu serikali kwa kutowahakikishia raia usalama wao hata baada ya kisa hicho kutokea.
“Inasikitisha, hata baada ya uvamizi huo, hatua zozote za kuwahakikishia wenyeji usalama wao hazijachukuliwa wala hakuna afisa wa serikali au kaunti aliyetembelea eneo la tukio. Ingawa mahala pa mauaji ni umbali wa kilomita nne pekee kutoka kituo cha polisi, hakuna jitihada zozote zinafanywa na walinda usalama kuwanasa wahalifu hao,” Bw Wario akaeleza wanahabari jijini Nairobi.
Vifo vya wazee hao vilitokea wakati mkutano wa amani kati ya wazee kutoka jamii za Gabra na Borana katika eneo la Forole ulivamiwa na wahalifu waliojihami vikali kutoka Ethiopia.
Wahalifu hao wanaaminika kutoka jamii ya Borana nchini Ethiopia na inadaiwa mkutano huo ulitumika kama chambo cha kuwahadaa wazee kutoka upande Wakenya ili wahalifu hao wawaue. Mzozo wa lishe ya mifugo pia ulitajwa kama sababu ya kutokota kwa uhasama kati ya Waborana na Wagabra.
Bw Wario pia alitoa wito kwa vyombo vya sheria kumchunguza Gavana wa Marsabit Mohamed Mahmud Ali kuhusiana na uvamizi huo.
Wazee waliofariki kutokana na mapigano ya juzi ni Budha Mamo, Dido Koke, Galgalo Khafo, Roba Wario, Elema Girgira, Dulacha Mamo, Boya Elema, Wario Elema, Dub Galgallo, Boru Elema na Boru Chuute.