Habari njema kwa Kenya 22 wakipona coronavirus
Na VALENTINE OBARA
JUMLA ya watu 22 walioambukizwa virusi vya corona walikuwa wamepona kufikia jana humu nchini.
Hali hii imeongeza matumaini kuhusu uwezo wa Kenya kukabiliana kikamilifu na virusi hivyo ikiwa wananchi wataendelea kufuata kanuni na masharti yanayotolewa na serikali.
Katika hotuba ya kila siku ya serikali kwa taifa kuhusu janga hilo, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, alisema kuna watu 10 waliothibitishwa kupona jana, na hivyo basi kuongeza idadi ya waliopona hadi 22.
Watu hao 10 ambao sasa wataruhusiwa kwenda nyumbani kutoka Hospitali ya Mbagathi, walifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu mara mbili kama inavyohitajika ili kuthibitisha kikamilifu kwamba wamepona.
Hayo yalijiri huku idadi ya walioambukizwa virusi hivyo ikiongezeka hadi 189 baada ya watu wengine watano kuthibitishwa wanaugua.
“Wote watano ni raia wa Kenya. Kati yao, ni mmoja pekee ambaye alikuwa amesafiri kutoka Uarabuni,” akasema Bw Kagwe akiongeza kuwa wengine walipatikana kwa juhudi za maafisa wa afyanchini.
Watatu kati ya watano hao ni kutoka Mombasa, mmoja Nairobi na mwingine Nyandarua. Kati yao, wawili ni wanaume na watatu ni wanawake. Umri wa wagonjwa hao ni kati ya miaka 27 na 58.
Bw Kagwe aliwasihi wananchi wajiepushe kutumia sarafu kwani huwa zinasambaza sana virusi vya corona.
Ni kwa msingi huu ambapo serikali ilishirikiana na mashirika ya kifedha na yale ya utoaji huduma za pesa kwa simu kupunguza gharama ya kutumia pesa kidijitali.
Wakati huo huo, alitangaza kwamba serikali sasa ina uwezo wa kupima watu 600 kwa siku moja.
Waziri alisema shughuli ya kupima watu wengi ilianza jana, na wahudumu wa afya wakapewa kipaumbele.
Ilibainika kuna uwezekano wahudumu wa afya hutangamana na wagonjwa wa corona bila kujua, baada ya watu wawili kufariki kwa magonjwa mengine kisha ikapatikana walikuwa wameambukizwa corona bila kujua.
Kaimu Mkurugenzi wa Afya ya Umma Dkt Patrick Amothm alisema kuanzia sasa itakuwa ni lazima mtu anayeugua nimonia apimwe pia ikiwa ameambukizwa virusi vya corona.
Alisema wale waliohudumia watu hao wawili ambao mmoja wao alikuwa mtoto, sasa wametengwa kwa siku 14 huku waliotangamana nao wakitafutwa.