Habari Mseto

Harambee Stars katika kikaango cha vigogo Ivory Coast Jumanne

June 11th, 2024 1 min read

NA CECIL ODONGO

KENYA leo inakabiliwa na mlima wa kukwea katika kufufua matumaini yake ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, itakapovaana na mabingwa wa Afrika, Cote d’Ivoire maarufu Ivory Coast, jijini Lilongwe, Malawi.

Mechi hiyo ambayo imesawiriwa kama vita kati ya Goliath na Daudi kwenye Bibilia, inatarajiwa kuanza saa 10 mchana kwenye uga wa Bingu jijini Lilongwe Malawi.

Itakuwa mara ya kwanza Kenya itachuana na Cote d’Ivoire katika soka.

Mashabiki wa soka wanatarajia burudani ya aina yake na watafuatilia mtanange huo kupitia runinga ya taifa ya KBC.

Chini ya kocha Engin Firat, Harambee iliwavunja wengi nyoyo Ijumaa iliyopita baada ya kutoka sare ya 1-1 na wanyonge Burundi katika mechi ya Kundi F.

Matokeo hayo yaliacha Harambee na Swallows zikiwa na alama nne, mbili nyuma ya Gabon nao viongozi Cote d’Ivoire wana alama tisa.

Gambia wana alama tatu, huku Ushelisheli ikiwa haina alama yoyote.

Kenya, ambayo inashikilia nafasi ya 107 kwenye viwango vya ubora vya Fifa, inaonekana kama mpinzani mswaki kwa Cote d’Ivoire.

Chini ya kocha Emerse Fael, Cote d’Ivoire iliishinda Gabon 1-0 wiki iliyopita na inatarajia kuwa itadumisha ubabe wake kwa kuzoa alama zote leo.

Firat alilalamika kuwa kupata sare dhidi ya Burundi kulichangiwa na kuwakosa wanasoka wawili wa kigeni ambao alikuwa akitarajia kuwatumia mchezoni.

Leo, bado Firat atawakosa mabeki Tobias Knost na Zak Vyner kwa kuwa mchakato wa kuhakiki stakabadhi za wanasoka hao ili waichezee Kenya bado haujakamilika.

“Lazima tubadilishe mbinu yetu ya kucheza na pia tutumie nafasi zetu. Ni mechi ambayo itatulazimu kushambulia na kuipiga jeki ulinzi wetu kwa sababu wapinzani wetu wana washambuliaji wakali,” akasema Firat.

Kocha huyo aliwaita kikosi David Okoth na David ‘Cheche’ Ochieng’ kwenye kikosi chake akilenga kuwatumia wanasoka hao kwenye mtanange wa leo.