Harusi haitoshi, kulingana na sheria, ndoa inathibitishwa kwa tendo chumbani
Na BENSON MATHEKA
JE, unafahamu kuwa mume au mkeo anaweza kukutaliki kwa kukosa kumtimizia haki yake ya tendo la ndoa?
Je, wajua kwamba ukikosa kushiriki tendo la ndoa kwa muda wa miezi mitatu baada ya harusi yako hapo hakuna ndoa.
Naam, kukosa kufanya tendo la ndoa na mume au mkeo katika muda wa miezi mitatu, muungano wenu hauwezi kutambuliwa kama ndoa.
Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, kususia tendo la ndoa kwa muda wa miezi mitatu baada ya harusi ni kukosa kutimiza hitaji la kufanikisha muungano wa mwanamume na mwanamke ili uitwe ndoa.
Hivyo basi, harusi inaweza kuwa ya kukata na shoka lakini ili kuifanikisha, ni lazima mtu na mkewe washiriki tendo la ndoa ndani ya miezi mitatu baada ya kuunganishwa kuwa mume na mke.
Kulingana na sheria ya Kenya, ndoa isiyoshirikisha tendo la ndoa katika miezi mitatu inaweza kufutiliwa mbali na mahakama kwa msingi kuwa haijathibitishwa.
Hii inaonyesha kwamba sheria inatambua umuhimu wa tendo la ndoa kwa waliooana rasmi. Hivyo basi, harusi pekee sio dhihirisho la ndoa bali ni muungano unaopelekea ndoa halisi kupitia tendo lenyewe.
Hivyo basi, kabla ya kufanya harusi, ni lazima mtu awe tayari kumtimizia mchumba wake mahitaji yake ya tendo la ndoa.
Ni muhimu kukumbuka kuwa sheria inatilia mkazo mchango wa tendo la ndoa katika ndoa hivi kwamba inasema ni haki ambayo mtu hafai kumnyima mkewe au mumewe.
Vile vile, inafaa kufahamika kuwa kubatilishwa kwa ndoa kwa sababu ya wanandoa kukosa kulishana uroda miezi mitatu baada ya kuoana sio sawa na talaka.
Hii ni kwa sababu tofauti na talaka, watu wakikosa kufanya mapenzi katika kipindi cha miezi mitatu baada ya harusi, yao haiwezi kutambuliwa kama ndoa kumaanisha kuwa nguzo kuu ya ndoa ni tendo la ndoa.
Hata hivyo, haimaanishi mtu amlazimishe mchumba wake kumlisha uroda ikiwa hayuko tayari kufanya hivyo au kuna sababu za kutosha kuepuka tendo la ndoa.
Kwa mfano, mtu anaweza kuugua ghafla punde tu baada ya kufunga harusi na katika hali hii mchumba wake anaweza kumwelewa na kumpa muda wa kupona hadi aweze kuwa katika hali nzuri ya kumwandalia tendo la ndoa.
Lakini ikiwa mtu hawezi kabisa kutekeleza tendo la ndoa, basi miezi mitatu inatosha mume au mkewe kuchukua hatua ili ndoa hiyo itangazwe batili.