Habari MsetoMakala

Hatari nchi kugeuzwa jangwa kufuatia ukataji wa miti kiholela

March 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

KENYA inakabiliwa na hatari ya kugeuka jangwa ikiwa ukataji miti kiholela, uchomaji makaa na uzoaji changarawe mitoni utaendelea bila kuthibitiwa.

Wataalamu wa mazingira wanaonya kwamba kasi ambayo Wakenya wanakata miti inaangamiza misitu, kukausha vyanzo vya maji na kuathiri hali ya hewa.

Hofu ya wanamazingira ni kuwa ukataji miti unaendelea bila miti mipya kupandwa jambo ambalo ni hatari kwa mazingira katika nchi ambayo idadi ya watu inaendelea kuongezeka.

Dkt Isaac Kalua, mwanzilishi wa Shirika la Green Africa Foundation asema licha ya hali hiyo, Kenya imepiga hatua katika ukuzaji wa misitu.

“Uchomaji wa makaa ni kwa sababu ya watu kupata riziki. Serikali zinazopiga marufuku ukataji miti zinapaswa kuwapa wakazi njia mbadala za kupata riziki,” alisema.

Anahisi kwamba kuna haja ya nia nzuri kutoka kwa wanasiasa kulinda na kuimarisha misitu kama kubuni jopo kazi la kutafuta jinsi ya kulinda misitu.
Mnamo Jumatatu, naibu rais William Ruto alizindua jopo la watu kumi la kuchunguza jinsi misitu inavyosimamiwa.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, kila nchi inapaswa kuhakikisha ina asilimia 10 ya misitu  jambo ambalo wataalamu wa mazingira wanasema ni ndoto  Kenya.

Misitu mikubwa kote nchini imevamiwa na wafanyabiashara wanaokata miti kiholela kupasua mbao, kuchoma makaa na kupata mashamba bila kujali athari za vitendo vyao kwa mazingira.

 

Marufuku

Ni hali hii iliyofanya serikali ya kitaifa na serikali kadhaa za kaunti kupiga marufuku uchomaji wa makaa, upasuaji wa mbao na uzoaji wa changarawe mitoni.

“Huwezi kutenganisha miti na mito. Ni miti katika misitu inayofanya nchi kuwa na mito yenye maji. Miti ikikatwa, mito huwa inakauka na ikikauka, binadamu na wanyama hukosa maji,” asema mwanamazingira Simion Mutua wa shirika la Trees for Life.

Dkt Isaac Kalua analaumu wanasiasa kwa uharibifu wa misitu.

“Changamoto tulizo nazo ni za kisiasa, tunafaa kufuata mkondo wa sayansi ikiwa tutalinda misitu yetu, lakini matukio ya hivi majuzi yanaonyesha kuna nia njema kutoka kwa wanasiasa|” ashauri Dkt Kalua aliye mwenyekiti wa shirika la kusimamia vyanzo vya maji Kenya (KWTA).

Ripoti ya hali ya misitu iliyotolewa 2016 na aliyekuwa waziri wa mazingira Judi Wakhungu ilionyesha kuwa misitu Kenya ilipungua kutoka  ekari 4,670,866 mwaka wa 1990 hadi ekari 3,492,358  mwaka wa 2000.

 

Asilimia 7

Kufuatia juhudi za serikali ya Rais Mwai Kibaki, kiwango hicho kilipanda hadi ekari  4,137,701 mwaka wa 2010. Mwaka 2017, serikali ilisema kiwango cha misitu kilikuwa asilimia 7. Bw Kalua anasema mwaka huu Kenya imefikia asilimia 7.2 na ina uwezo wa kufikia asilimia 10.

Kulingana na ripoti hiyo, Kenya hupoteza Sh6 bilioni kwa sababu ya uharibifu wa misitu kila mwaka na kwamba asilimia 70 ya vyanzo vya  maji vinakabiliwa na hatari ya kuangamia.

Baadhi ya misitu mikubwa ambayo imeathiriwa na wakataji wa miti ni Mlima Kenya, Aberdares na Mau,  Mlima Elgon na Cherangani.

Kuna misitu 22 ambayo imesajiliwa na kuchapishwa kama vyanzo vya maji nchini. Hata hivyo, wanamazingira wanasema juhudi za kulinda misitu hutatizwa na maslahi ya kisiasa na ukosefu wa sera madhubuti za kuisimamia.

“Uharibifu wa misitu ili kuwavutia wapigakura unatatiza juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kufikia 2030,” aeleza.

 

Siasa

Afisa mmoja wa shirika la misitu ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa kuhofia kazi yake alisema juhudi za kulinda misitu Kenya zinaingizwa siasa. “Hii inafanya Kenya kualika ghadhabu ya hali ya hewa kama iliyoshuhudiwa kuanzia Desemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu.

Nina hakika tukiendelea kuingiza siasa katika masuala ya mazingira, Kenya itakuwa jangwa katika miaka michache ijayo,” alieleza afisa huyo.

Kufikia 2016, ni asilimia 7 ya Kenya iliyokuwa imepandwa miti. Ripoti  hiyo inafichua uharibifu wa misitu katika Mau, Mlima Kenya na msitu wa Marmanet ambao ulifanya maji katika mito mingi kupungua.

Inaeleza kwamba tisho kuu kwa misitu ni uvamizi,  watu kugawiwa ardhi ya misitu, makao haramu na ukataji miti kinyume cha sheria.
Ripoti iliangazia hali ya misitu katika maeneo ya Kati, Bonde la Ufa, Mashariki na Magharibi.