Habari Mseto

Hatima ya Jaji Ojwang mikononi mwa jopo la watu saba

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

HATIMA ya Jaji Jackton Boma Ojwang wa Mahakama ya Juu imo mikononi mwa jopo la watu saba ambao Rais Uhuru Kenyatta aliteua Jumanne kumchunguza kufuatia pendekezo la Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC).

Jopo hilo linalosimamiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Alnashir Visram litachunguza madai kwamba Jaji Ojwang alihusika na vitendo vilivyo kinyume na maadili ya kazi ikiwa ni pamoja na kupokea hongo.

Likipata ushahidi na kuridhika kwamba alitenda makosa, litapendekeza aondolewe wadhifa wa jaji na likikosa kumpata na hatia, ataendelea kuhudumu kama jaji wa Mahakama ya Juu.

Kwenye ilani katika gazeti rasmi la serikali, Rais Kenyatta alimteua Jaji Mstaafu Festus Azangalala, wakili Ambrose Weda, Andrew Bahati Mwamuye,Lucy Kambuni, Sylvia Wanjiku Muchiri na Amina Abdalla kuwa wanachama wa jopo hilo. Alisema alichukua hatua hiyo kufuatia pendekezo la JSC.

Bw Paul Nyamodi na Stella Munyi watakuwa mawakili wa kusaidia jopo hilo nao Peter Kariuki na Josiah Musili watakuwa makatibu.

Rais Kenyatta alisema kwamba Jaji Ojwang atasimamishwa kazi hadi jopo hilo litakapomaliza kumchunguza na kutoa mapendekezo yake.

Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) ilipendekeza jaji huyo kuchunguzwa kufuatia madai mbali mbali dhidi yake ikiwa ni pamoja na kupokea hongo ili apendelee upande mmoja kwenye uamuzi wa kesi.

Aidha, analaumiwa kwa kushirikiana na serikali ya Kaunti ya Migori na Gavana wa Okoth Obado.

Miongoni mwa madai dhidi ya Jaji Ojwang’ ni kwamba aliandika uamuzi katika kesi iliyohusu eneo la kupanda miwa la Sony na kisha akazawadiwa na Bw Obado.

Kulingana na walalamishi, Gavana Obado alijenga barabara inayoelekea katika boma la jaji huyo viungani mwa mji wa Migori hata kuweka taa kwenye barabara hiyo.

Kulingana na JSC, Ojwang angewafahamisha wahusika wakiwemo majaji alioshirikiana nao kusikiliza kesi hiyo kuhusu uhusiano wake na Bw Obado lakini hakufanya hivyo hadi wakalalamika.

Baadhi ya walalamishi ni wakazi wa Kaunti ya Homa Bay anakotoka Jaji Ojwang.

Tume ilisema ilipata kwamba madai hayo yana msingi na ikapendekeza Rais kuunda jopo la kumchunguza Jaji Ojwang kulingana na sheria.

Jaji Ojwang alikataa kufika binafsi mbele ya JSC na kutaja madai hayo kama ya kubuniwa. JSC ndiyo mwajiri wa majaji na maafisa wengine wa mahakama na huwa inapokea malalamishi kuhusu utendakazi wao na kuchunguza madai yote.

Baadhi ya wanachama wa jopo ni mawakili ambao wamewahi kufika mbele ya jaji huyo kuwakilisha wateja wao katika kesi mbali mbali.

Jopo hilo litaandaa vikao na kuwaita walalamishi, Ojwang mwenyewe na mashahidi iwapo wako, kufika mbele yake kabla ya kuandika ripoti itakayowasilishwa kwa rais ambaye atafuata mapendekezo yatakayotolewa.