Hatimaye Tanui ajisalimisha kwa polisi na kushtakiwa
NA RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA mkurugenzi mkuu wa shirika la kusambaza mafuta nchini (KPC) Bw Charles Kiprotich Tanui aliyeamriwa akamatwe kwa ufujaji wa zaidi ya Sh644 milioni za umma alishtakiwa Alhamisi baada ya kujisalamisha kwa polisi.
Bw Tanui alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo pamoja na washukiwa wengine sita.
Mabw Tanui , Philip Kimelu, Bramwel Juma Wanyalikha, Charles Ochieng Ouko, Fredrick Kagosh Ogenga, Francis Omondi Obure, Beryl Aluoch Khasinah na kampuni ya Aero Dispenser Valves walikanusha mashtaka ya ufisadi na utumiaji wa mamlaka vibaya.
Wote walikanusha shtaka la kufanya njama za kuifuja shirika la KPC Dola za Marekani 6,441,700 (Sh644 milioni).
Bw Ogenga aliyekuwa afisa wa ununuzi katika KPC alishtakiwa kwa kupeleka ujumbe kwa kampuni ya Allied Inspection & Testing Inc. kuhusu ujenzi wa bomba na kiwanda cha mafuta cha Kisumu Oil Jetty bila idhini ya kamati ya zabuni ya shirika hilo.
Bw Obure na Beryl ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Aero Dispenser walishtakiwa kwa kupelekea KPC barua iliyotolewa kwa msajili wa kampuni katika afisi ya mwanasheria mkuu (AG) ikiiunga mkono kuhusu kupewa zabuni ya kununua mitambo na mabomba ya kuwekeza katika mradi wa Kisumu Oil Jetty.
Pia Obure na Beryl walishtakiwa kwa kuwasilisha barua feki kwa KPC ikithibitisha Aero Dispenser imeteuliwa kuwakilisha kampuni ya Cla Val Company Limited iliyokuwa imepewa kandarasi ya kuweka mitambo na mabomba katika mradi wa Kisumu Oil Jetty na kuinunulia vipuri kwa muda wa miaka miwili.
Kampuni hiyo ya Aero , Obure na Khasinah walishtakiwa kwa kupokea kwa njia ya undanganyifu pesa za umma Dola za Marekani 2,546,076.31 (Sh254.6 milioni).
Washtakiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh2milioni isipokuwa Ogenga aliyepewa dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000.