Hatuna uwezo wa kukabili corona, kaunti sasa zalia
SHABAN MAKOKHA, ONYANGO K’ONYANGO na WANDERI KAMAU
KAUNTI zimeeleza wasiwasi kwamba huenda zikashindwa kudhibiti mikakati ya kukabili maambukizi ya virusi vya corona, ambapo sasa zinaomba usaidizi wa Serikali ya Kitaifa.
Hili linajiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kufanya kikao maalum na magavana wote 47 nchini kwenye Ikulu mnamo Jumatano, kujadili kuhusu mikakati ya kujitayarisha kukabili virusi hivyo.
Gavana Sospeter Ojaamong wa Busia ameeleza wasiwasi kuhusu uwezo wa kaunti kukabili janga hilo, akisema kuwa kaunti yake imemaliza nafasi za kuwahifadhi watu wanaothibitishwa kuambukizwa virusi.
Bw Ojaamong alitaja uhaba wa Vifaa vya Kujilinda (PPEs) kama changamoto kuu inayoikabili serikali yake kwenye harakati za kukabili virusi.
Alisema kuwa tayari, kaunti imemaliza kutumia fedha ambazo ilitengewa na serikali kuimarisha juhudi hizo.
Hii ni baada ya kutengeneza vituo viwili ambavyo vina vitanda 242.
Tayari, Serikali ya Kitaifa imetengea kaunti Sh5 bilioni ili kuimarisha juhudi hizo.
Awali, kaunti hiyo ilikuwa imetenga chumba chenye vitanda 71 katika kituo cha Alupe lakini idadi ya wale walioambukizwa imeongezeka na kuzidi idadi hiyo.
Kaunti hiyo imeongeza Shule ya Upili ya St Monicah Chakol ambayo ina vitanda 200 na Kituo cha Chakol cha Mafunzo ya Kilimo ambacho kina vitanda 42.
“Tunafanya mazungumzo na Serikali ya Kitaifa kukifanya Chuo cha Mafunzo ya Matibabu (KMTC) Busia kuwa karantini ili kuongeza nafasi ya kuwahifadhi watu wanaothibitishwa kuambukizwa,” akasema.
Na katika Kaunti ya Uasin Gishu, wakazi na wanasiasa wanaitaka serikali ya kaunti kueleza wazi ikiwa ina nafasi za kutosha kuwahifadhi watu ambao watabainika kuambukizwa.
Hili ni kutokana na ongezeko la visa vya virusi katika kaunti hiyo.
Hapo jana, mbunge wa Ainabkoi, William Chepkut na baadhi ya wakazi walimtaka Gavana Jackson Mandago kuwahakikishia wakazi ikiwa kuna vitanda vya kutosha katika kaunti hiyo.
Mbunge huyo alisema hali ya unyamavu katika serikali hiyo kuhusu hali ya vitanda ni ishara tosha kuwa huenda hali si nzuri.
Malalamishi hayo yanajiri huku idadi ya virusi hivyo kote nchini ikifikia 3, 215 baada ya watu 124 zaidi kuthibitishwa kuambukizwa jana.
Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa visa 49, Busia (37), Mombasa (20) kati ya kaunti zingine.
Hata hivyo watu 44 waliruhusiwa kwenda nyumbani, hilo likifikisha idadi ya waliopona kuwa 1,092.
Watu watatu zaidi walifariki na kufikisha idadi ya waliofariki kuwa 92.Mnamo Jumatano, Serikali ilizindua rasmi kanuni za kutumiwa kutibu watu wanaopatikana na virusi vya corona wakiwa nyumbani katika juhudi za kupunguza msongamano katika vituo vya serikali vya kutenga na kutibu wagonjwa.
“Kufuatia idadi kubwa ya watu wanaothibitishwa kuwa na virusi hivi nchini, serikali haitaweza kuwahifadhi wagonjwa wote katika vituo vyake. Kuzinduliwa kwa kanuni hizi kunamaanisha kuwa mfumo huu utaanza kutumika mara moja,” akasema Dkt Aman.
Kulingana na kanuni za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) mgonjwa aliye na virusi vya corona, anafaa kuwekwa katika chumba kilichotengwa ambacho kina hewa ya kutosha. Kanuni zinasema mgonjwa akiwa katika chama hicho, hafai kutembelewa na watu isipokuwa wahudumu wa afya.