Habari MsetoSiasa

Hatuwezi kuvumilia kuona mauaji ya kinyama kila siku – Uhuru

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alivunja kimya chake kuhusu visa vya mauaji ya kiajabu vinavyoripotiwa humu nchini.

Aliwataka maafisa wa usalama kukomesha mauaji hayo ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika maeneo mbalimbali katika siku za hivi karibuni.

Rais Kenyatta akitoa amri hiyo alipotuma risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago kufuatia kisa cha kakake mkubwa.

Mwili wa John Mandago ulipatikana katika chumba kimoja cha malazi katika mtaa wa Chepkanga, mjini Eldoret mnamo Jumatatu jioni bila alama zozote.

Alikuwa amewaambia watu wa familia yake kwamba alikuwa ameenda mjini Kapsabet, kaunti ya Nandi.

Kifo hicho kilithibitishwa na Naibu Kamishna wa Kaunti Lilian Langat huku akiahidi kuwa polisi watafanya uchunguzi kubaini kilimuua.

Katika risala zake Rais Kenyatta alisema kuwa visa vya mauaji ya watu wasio na hatia vinatamausha na Idara ya polisi inapasa kuchukua hatua kuvikomesha.

“Sharti tubaini chanzo cha mauaji hayo ya kikatili. Hatuwezi kuvumilia mauaji kama haya kila siku. Hali haitakubalika,” Rais Kenyatta akasema.

“Maafisa wetu wa usalama wanafaa kuchukua hatua za haraka kukomesha mauaji haya. Tutumia rasilimali zetu zote kuwahakikishia Wakenya usalama wao kote nchini,” akaongeza.

Wito wa Rais Kenyatta umejiri wakati ambapo visa vya mauaji tata ya wanaume na wanawake kuuawa kinyama huku wengine wajitoa uhai.

“Hatuwezi kuruhusu wahalifu wachache kuendelea. Mauaji ya hivi majuzi katika eneo bunge la Matungu, Marsabit na maeneo mengine nchini ni ya kusikitisha,” akaendelea kusema.

Zaidi ya watu 21 wameuawa tangu magenge ya wahalifu yaanze kuwahangaisha wakazi wa Matungu, kaunti ya Kakamega mapema mwezi huu.

Na katika maeneo mengine nchini watu kadhaa wameaua katika mavamizi ya wezi wa mifugo, tofauti za kimapenzi na mtafaruku katika ndoa.