Habari Mseto

Heroini: DPP ataka mshukiwa aozee jela miaka miaka 22

January 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA BRIAN OCHARO

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji anataka mfanyabiashara ambaye anatumikia kifungo cha miaka 22 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha heroini ya Sh30 milioni anyimwe dhamana kwa hofu kuwa anaweza kutoroka.

Ahmed Said Bakar amekata rufaa dhidi ya kifungo hicho, na anataka Mahakama ya Juu kumwchilia kwa dhamana akisubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa rufaa ya kifungo chake.

Lakini DPP kupitia Kwa Kiongozi wa mashtaka Jami Yamina anapinga ombi la Bw Bakari kwa hofu kuwa kuna uwezekano mshukiwa huyo anatafuta njia za kutoroka.

“Bw Bakari anatumikia kifungo cha miaka 20 pamoja na faini ya Sh8million au kifungo cha miaka miwili gerezani akishindwa kulipa faini hiyo. Faini hizo hazijalipwa, tunahofia mshukiwa anatafuta njia ya kutoroka ili kuchelewesha kesi hii,” alisema.

Mwendesha mashtaka pia alisema kuwa mshukiwa hajaeleza kwa kutoa ushahidi iwapo mahakama itakubaliana na ombi la kubatilisha kifungo dhidi yake na kuongezea kuwa hakuna sababu za kipekee zimetolewa kuunga mkono ombi la kutaka kupewa dhamana.

Bw Yamina alisema kumuachilia kwa dhamana mshukiwa ndani ya miezi miwili baada ya kuhukumiwa itaathiri vita dhidi ya mihadarati na pia itafanya wakenya wasiwe na imani na mahakama.

DPP pia ameomba mahakama kutupilia mbali rufaa ya Bw Bakari.

Bw Bakari anasema katika rufaa yake kuwa alishtakiwa na kuhukumiwa kwa karatasi ya mashtaka ambayo ina makosa na kwamba alifungwa jela kwa tuhuma tu, ambayo haikuthibitishwa na ushahidi wa kushawishi.

“Matokeo ya uchunguzi uliotumika katika kesi hii hayakuungwa mkono na ushahidi wowote,” alijitetea hasa kuhusiana na umiliki wa sanduku ambalo dawa za kulevya zilipatikana,” alisema katika karatasi zake za mahakama.

Bw Bakari alifungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya biashara ya kusafirisha madawa ya kulevya, ambayo ilikuwa inasafirishwa Madagascar.

Lakini Bw Bakari sasa anataka hukumu hiyo ibatilishwe , anataka pia Jaji wa Mahakama ya Juu Njoki Mwangi kumpa dhamana huku akisubiri kumalizika kwa rufaa yake. Bw Bakari alifungwa pamoj na Clement Serge Bristol, raia wa Sychelles ambaye alihukumiwa miaka 10 na kupigwa faini ya ziada ya Sh5millioni.

Bw Bakari anakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha gramu 2028 ya heroini ya thmani ya milioni sita zikiwa zimefichwa kwenye mfuko wa kusafiria ambayo ilikuwa imewekwa kwenye buti la gari.

Pia anashtakiwa kwa kusafirisha kwa kupitisha gramu 7,600 ya heroini ya thamani ya Sh22.8millioni zikiwa zimefichwa ndani ya tangi la meli ndogo kwa jina Baby Iris.

Upande wa mashtaka unasema mshukiwa alifanya makosa hayo mnamo Aprili 9,2015 huko Mnarani katika kaunti ya Kilifi.

Lakini Bw Bakari sasa anataka mahakama ya rufaa kubatilisha uamuzi wa mahakama ya mahakimu akisema alifungwa kwasababu ya uhusiano wake na mwenye meli hiyo .