Himizo watoto wafuatilie madrassa kwa redio
Na BRENDA AWUOR
WAISLAMU katika Kaunti ya Kisumu wamehimizwa wahakikishe watoto wao wanategemea kituo kimoja cha redio, ambacho kitaendeleza masomo ya madrassa wakati huu ambapo misikiti na madrasa yamefungwa.
Mwenyekiti wa chama cha Waislamu Kisumu, Sheikh Musa Hajji, alisema masomo hayo pamoja na mahubiri yataendelea, lakini kupitia kwa redio.
“Sisi tumetii agizo la serikali kwamba misikiti ifungwe. Tunajua watoto wetu wamekuwa wakisomea madrassa kwenye misikiti. Kwa hivyo nawashauri wazazi wahakikishe watoto wao wanafuatilia mafunzo haya kupitia kituo cha Peace FM,” akasema.
Kituo hicho ni cha Kiislamu ambacho matangazo yake huangazia mawaidha ya kidini miongoni mwa vipindi vingine.
Sheikh Hajji alikuwa akizungumza katika msikiti wa Jamia Kisumu, ambapo alifafanua kuwa mafunzo yote ya kidini sasa yatakuwa kwa njia ya redio pekee.
Hali hiyo inatarajiwa kuendelea hadi virusi vya corona vitakapotangazwa kuwa si tisho tena kwa Wakenya.Aidha, alisema kuswali nyumbani ni jambo linalohimizwa na mafunzo ya Uislamu nyakati za dharura.
“Bwana Mtume ametufunza kuwa hata kunapokuwa na mvua na mtu hawezi kufika msikitini, anaruhusiwa aswali kwake nyumbani. Janga hili ni kubwa kuliko Baraka ya mvua. Nawahimiza Waislamu tuswali mwetu majumbani wakati huu,” akasema.
Kuhusu swala kwa maiti, alisema sasa hivi watu watakuwa wakiswalia wafu wao majumbani.“Kati ya mambo ya lazima kufanyiwa marehemu, ni kuoshwa, kuvikwa sanda na kuswaliwa.
Swala hii si lazima tuifanye msikitini. Inaweza kufanywa na watu wa familia kama ilivyoagiza serikali kuhusu mikusanyiko,” akasema.
Aliahidi kuwa chama chake kitaendelea kugawa sabuni ya kusafisha mikono katika maeneo mengine ya Kisumu. Eneo la kwanza kunufaika na mpango huo ni Kaloleni.