Hisia, mapenzi yanapoisha ni sababu tosha ya kuvunja ndoa, korti
MAHAKAMA moja jijini Nakuru imetoa uamuzi kuwa mapenzi na hisia kati ya wanandoa zinapokatika, ni sababu tosha ya kujiondoa katika ndoa hiyo.
Jaji Samuel Mohochi alitoa uamuzi huo katika kesi ya talaka inayohusu wanandoa wenye asili ya Kihindi ambao hawapendani tena.
Jaji huyo alisema, iwapo mapenzi yameisha, mwanandoa yeyote hapaswi kufungwa na kanuni za kisheria wala za kidini.
“Hakuna mwanamume au mwanamke anayeweza kufungwa na sheria au dini katika hali ambapo hakuna mapenzi au hisia, kudumisha uhusiano wa ndoa,” alisema Jaji Mohochi.
Alisema ndoa ambayo mapenzi na hisia kati ya wanandoa yameisha, inaweza kuchukuliwa kama iliyovunjika kwa sababu hakutakuwa na kinachowashikilia wawili hao pamoja.
Aliruhusu Bw NHS kumpa talaka mkewe Bi TSS waliyeishi naye kwa miaka 20 na ambaye alimshutumu kuwa mdhalimu na mvivu ilhali anaitisha maisha ya kifahari.
Bw NHS alidai mke wake amemwitisha mengi kupindukia lakini hataki kuchangia katika utajiri wa familia.
Katika kesi aliyowasilisha kortini, NHS alisema mke wake huzua vurugu, ni mwingi wa matusi na ni mgomvi kila anapoitisha anayotaka.
Korti ilisikia kuwa mwanamke huyo alichukua dhahabu ya familia, akafuja karibu Sh 25 milioni alizopatiwa na kuanza kukopa huku akiendelea kumshambulia na kumuumiza mume wake kisaikolojia.
“Kuharibu mambo zaidi, amezidi kumvamia mlalamishi kwa kumfuata kazini akimrushia cheche za matusi mbele ya wateja na wafanyakazi hivyo basi kumshushia hadhi na kumsababishia mlalamishi wasiwasi na uchungu mwingi kimawazo,” alieleza Bw NHS.
Hata hivyo, mkewe, akijibu kesi hiyo, alikanusha shutuma zilizotolewa na mume wake aliyedai ni msherati.
Alieleza korti kuwa mume wake aliondoka boma lao kwa hiari na kutoroka na mke wa mwanamume mwingine kabla ya kukodisha nyumba iliyopo ghorofa moja juu yao.
Alisema amemkabili mume wake mara kadhaa kuhusu alichotaja kama misururu ya mahusiano nje ya ndoa ambayo hangeweza kustahimili.
“Hakuna mke wala mume anayeweza kustahimili mwanandoa mwenzake ambaye ni mzinzi au ana mahusiano nje ya ndoa katika sayari hii au kwingineko,” alisema.
Bi TSS alimshutumu mume wake kwa kukosa kutunza familia yao kwa sababu alikuwa analipa kodi pekee ilhali alikuwa anampa Sh30,000 kila mwezi kwa matumizi ya familia.
Alifafanua kuwa aliacha kazi yake ili kumtunza mtoto wao, kutunza boma na kumtunza baba mkwe wake aliyekuwa akiugua kabla ya kuaga dunia miaka sita iliyopita.
Nakala za korti zilionyesha kuwa wawili hao walifunga ndoa Julai 2002 kuambatana na sheria iliyovunjiliwa mbali kuhusu Ndoa na Talaka ya Kihindi.
Walijaaliwa mtoto mmoja mnamo Februari 20,2006, na kisha wakatengana 2020 mume alipohama boma lao.