Hitilafu za vifaa kwenye uchaguzi mdogo Baringo Kusini
Na PETER MBURU
SHUGHULI za uchaguzi mdogo wa eneobunge la Baringo Kusini zilianza Ijumaa alfajiri, huku visa vya baadhi ya vifaa vya kuendesha uchaguzi kuwa na hitilafu vikiripotiwa.
Saa za asubuhi bado zilishuhudia idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura, huku kukiwa na matarajio kuwa idadi hiyo ingeongezeka kadri siku ilivyokua.
Baadhi ya vituo vilivyoadhiriwa na kufeli kwa vifaa hivyo vya uchaguzi ni pamoja na kile cha shule ya upili ya Marigat na kituo cha Kimorok.
Watu wa eneobunge hilo walilazimika kurejea katika uchaguzi baada ya mbunge waliyemchagua mwaka uliopita Bi Grace Kipchoim kuaga dunia Aprili 2018.
Wale wanaobishania kiti hicho ni Charles Kamuren kwa chama cha Jubilee, Cynthia Kipchilat wa Maendeleo Chap Chap, Paul Kimaru Motoloi kwa tiketi ya Chama Cha Mashinani na Sylvester Sergon wa Republican Labour Party.
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) Bw Wafula Chebukati alishuhudia uchaguzi huo akiwa katika eneobunge hilo.
Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kutoka kwa mmoja wa wagombeaji kuwa kunao waliowahonga watu ili wawapigie kura.
Lakini maafisa wa IEBC waliwahakikishia wakazi kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na kuwa utakuwa huru na wa haki.